Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 22:14-21 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Ahimeleki akamjibu, “Kati ya watumishi wako, Daudi ndiye ofisa wa kuaminika kuliko wote. Yeye ni mkwe wako wewe mfalme mwenyewe, kapteni wa kikosi chako cha ulinzi na anaheshimika kuliko wote nyumbani mwako.

15. Leo, sio mara ya kwanza kumwomba Mungu shauri kwa ajili yake. Mfalme, usinishuku mimi wala mtu yeyote katika jamaa ya baba yangu juu ya njama hizo. Mimi mtumishi wako, sijui lolote, liwe kubwa au dogo juu ya jambo hilo.”

16. Lakini mfalme Shauli akamwambia, “Ahimeleki, hakika utauawa, wewe na jamaa yote ya baba yako.”

17. Shauli akawaambia walinzi waliokuwa wamesimama kandokando yake, “Geukeni na kuwaua makuhani wa Mwenyezi-Mungu, maana wao wanapatana na Daudi; walijua kuwa ametukimbia wala hawakuniarifu.” Lakini walinzi hao hawakuinua mikono yao ili kuwaua makuhani wa Mwenyezi-Mungu.

18. Kwa hiyo, mfalme Shauli akamwambia Doegi, “Wewe geuka ukawaue makuhani.” Doegi, Mwedomu, akaenda na kuwaua makuhani wote. Siku hiyo, Doegi aliua makuhani themanini na watano ambao huvaa vizibao vya kikuhani vya kitani.

19. Kisha aliwaua kwa makali ya upanga wakazi wote wa Nobu, mji wa makuhani, wanaume na wanawake, watoto wadogo na wanyonyao, ng'ombe, punda na kondoo.

20. Lakini Abiathari, mmoja wa watoto wa kiume wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, aliponyoka akakimbilia kwa Daudi.

21. Abiathari alimweleza Daudi kuwa Shauli amewaua makuhani wa Mwenyezi-Mungu.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 22