Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 20:9-17 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Yonathani akamjibu, “Wazo hilo na liwe mbali nawe. Hakika, kama ningejua kuwa baba yangu amekusudia mabaya juu yako nisingekuficha.”

10. Daudi akauliza, “Nitajuaje ikiwa baba yako atakujibu kwa ukali?”

11. Yonathani akamjibu, “Njoo twende shambani!” Basi, wakaenda.

12. Yonathani akamwambia Daudi, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, na awe shahidi yetu. Kesho au kesho kutwa, wakati kama huu nitamwuliza baba yangu. Ikiwa msimamo wake juu yako ni mzuri nitakueleza.

13. Mwenyezi-Mungu na aniue ikiwa Shauli anakusudia kukudhuru, nami nisikutahadharishe ili uende mahali mbali ambapo utakuwa salama. Mwenyezi-Mungu na awe pamoja nawe kama alivyokuwa pamoja na baba yangu.

14. Ikiwa nitaendelea kuwa hai basi, nioneshe ule upendo thabiti wa Mwenyezi-Mungu, ili nisife,

15. tena usiache kuitendea jamaa yangu kwa uaminifu milele. Na Mwenyezi-Mungu atakapowakatilia mbali adui zako kutoka duniani,

16. naomba na jina langu lisikatiliwe mbali kutoka jamaa yako. Mwenyezi-Mungu awalipize kisasi adui zako.”

17. Kwa mara nyingine tena, Yonathani alimwambia Daudi aape kulingana na upendo wake kwake yeye Yonathani, kwani alimpenda Daudi kama alivyoipenda roho yake.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 20