Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 19:16-24 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Wale watu walipoingia nyumbani kwa Daudi na kukiangalia kitanda waliona kuna kinyago na mto wa manyoya ya mbuzi kichwani.

17. Halafu Shauli akamwuliza Mikali, “Kwa nini umenidanganya? Umemwacha adui yangu atoroke?” Naye Mikali akamjibu Shauli, “Aliniambia, ‘Niache niende nisije nikakuua.’”

18. Daudi alipotoroka, alikwenda Rama kwa Samueli. Alimweleza Samueli mambo yote aliyomfanyia Shauli. Basi, Daudi na Samueli walikwenda na kukaa huko Nayothi.

19. Baadaye Shauli aliambiwa kuwa Daudi alikuwa huko Nayothi katika Rama.

20. Ndipo Shauli alipopeleka watu wakamkamate. Lakini walipolikuta kundi la manabii likitabiri na Samueli akiliongoza, roho ya Mungu iliwajia wale watumishi wa Shauli, nao pia wakaanza kutabiri.

21. Shauli alipoambiwa habari hizo, alituma watumishi wengine, nao pia wakaanza kutabiri. Shauli alipotuma watumishi wengine kwa mara ya tatu, nao pia wakaanza kutabiri.

22. Ndipo yeye mwenyewe akaenda Rama. Alipofika kwenye kisima kikubwa kilichoko huko Seku, alimkuta mtu fulani ambaye alimwuliza, “Samueli na Daudi wako wapi?” Huyo mtu alimjibu, “Wako Nayothi, katika Rama.”

23. Naye Shauli akaenda huko Nayothi katika Rama. Alipofika huko, roho ya Mungu ilimjia, naye alianza kutabiri akiwa njiani mpaka alipofika Nayothi katika Rama.

24. Alivua mavazi yake akawa anatabiri mbele ya Samueli. Alibaki uchi kwa siku moja, mchana na usiku. Kwa hiyo watu walianza kujiuliza, “Je, Shauli naye pia amekuwa mmoja wa manabii?”

Kusoma sura kamili 1 Samueli 19