Sura

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
  17. 17
  18. 18
  19. 19
  20. 20
  21. 21
  22. 22
  23. 23
  24. 24
  25. 25
  26. 26
  27. 27
  28. 28
  29. 29
  30. 30
  31. 31

Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 19 Biblia Habari Njema (BHN)

Shauli anamwandama Daudi

1. Shauli alimweleza mwanawe Yonathani na maofisa wake juu ya mpango wake wa kumwua Daudi. Lakini Yonathani, mwanawe Shauli, alimpenda sana Daudi.

2. Kwa hiyo, akamwambia, “Baba yangu anakusudia kukuua. Hivyo, jihadhari. Kesho asubuhi, jifiche mahali pa siri, ukae hapo.

3. Mimi nitakuja na kusimama karibu na baba yangu huko shambani mahali utakapokuwa. Hapo nitaongea naye juu yako, na kitu chochote nitakachogundua kutoka kwake, nitakueleza.”

4. Yonathani alimsifu Daudi mbele ya baba yake, akamwambia, “Usitende dhambi dhidi ya mtumishi wako Daudi kwani yeye hajatenda dhambi yoyote dhidi yako; matendo yake yote anapokutumikia daima yamekuwa mema kwako.

5. Alipomuua yule Mfilisti Goliathi, alihatarisha maisha yake, naye Mwenyezi-Mungu aliwapa Waisraeli ushindi mkubwa. Wewe ulipoona jambo lile ulifurahi. Kwa nini unataka kutenda dhambi kwa kumwaga damu isiyo na hatia kwa kumwua Daudi bila sababu?”

6. Shauli alimsikiliza Yonathani, kisha akaapa, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, sitamuua Daudi.”

7. Hivyo, Yonathani akamwita Daudi na kumweleza mambo hayo yote. Yonathani akampeleka Daudi kwa Shauli, na Daudi akamtumikia Shauli kama hapo awali.

8. Baadaye kulikuwa na vita tena kati ya Wafilisti na Waisraeli. Daudi alitoka akapigana na Wafilisti, akawaua Wafilisti wengi na waliosalia wakamkimbia.

9. Kisha, roho mbaya kutoka kwa Mwenyezi-Mungu alimjia Shauli alipokuwa amekaa nyumbani kwake akiwa ameshika mkuki mkononi, wakati ambapo Daudi alikuwa akipiga kinubi.

10. Shauli alijaribu kumchoma Daudi kwa mkuki huo, Lakini Daudi alikwepa mkuki wa Shauli na mkuki ukapiga ukuta. Daudi akakimbia na kutoroka.

11. Usiku huo, Shauli alituma watu nyumbani kwa Daudi wamwangalie kama yuko ili apate kumwua asubuhi. Lakini Mikali, mke wa Daudi akamwambia Daudi, “Kama huyasalimishi maisha yako usiku huu kesho utauawa.”

12. Hivyo Mikali akamteremsha Daudi kupitia dirishani, naye akatoka na kutoroka.

13. Mikali akachukua kinyago, akakilaza kitandani na kichwani pake akaweka mto wa manyoya ya mbuzi. Kisha akakifunika kwa nguo.

14. Shauli alipotuma watu kumshika Daudi, Mikali akawaambia kuwa Daudi ni mgonjwa.

15. Kisha Shauli aliwatuma warudi huko tena, akawaagiza akisema, “Mlete kwangu Daudi hata akiwa kitandani ili auawe.”

16. Wale watu walipoingia nyumbani kwa Daudi na kukiangalia kitanda waliona kuna kinyago na mto wa manyoya ya mbuzi kichwani.

17. Halafu Shauli akamwuliza Mikali, “Kwa nini umenidanganya? Umemwacha adui yangu atoroke?” Naye Mikali akamjibu Shauli, “Aliniambia, ‘Niache niende nisije nikakuua.’”

18. Daudi alipotoroka, alikwenda Rama kwa Samueli. Alimweleza Samueli mambo yote aliyomfanyia Shauli. Basi, Daudi na Samueli walikwenda na kukaa huko Nayothi.

19. Baadaye Shauli aliambiwa kuwa Daudi alikuwa huko Nayothi katika Rama.

20. Ndipo Shauli alipopeleka watu wakamkamate. Lakini walipolikuta kundi la manabii likitabiri na Samueli akiliongoza, roho ya Mungu iliwajia wale watumishi wa Shauli, nao pia wakaanza kutabiri.

21. Shauli alipoambiwa habari hizo, alituma watumishi wengine, nao pia wakaanza kutabiri. Shauli alipotuma watumishi wengine kwa mara ya tatu, nao pia wakaanza kutabiri.

22. Ndipo yeye mwenyewe akaenda Rama. Alipofika kwenye kisima kikubwa kilichoko huko Seku, alimkuta mtu fulani ambaye alimwuliza, “Samueli na Daudi wako wapi?” Huyo mtu alimjibu, “Wako Nayothi, katika Rama.”

23. Naye Shauli akaenda huko Nayothi katika Rama. Alipofika huko, roho ya Mungu ilimjia, naye alianza kutabiri akiwa njiani mpaka alipofika Nayothi katika Rama.

24. Alivua mavazi yake akawa anatabiri mbele ya Samueli. Alibaki uchi kwa siku moja, mchana na usiku. Kwa hiyo watu walianza kujiuliza, “Je, Shauli naye pia amekuwa mmoja wa manabii?”