Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 17:23-31 Biblia Habari Njema (BHN)

23. Alipokuwa anaongea nao, Goliathi yule shujaa wa Wafilisti kutoka Gathi alijitokeza mbele ya wanajeshi wa Israeli kama alivyozoea. Naye Daudi alimsikiliza vizuri sana.

24. Waisraeli walipomwona Goliathi, walimkimbia, na kumwogopa sana.

25. Waliambiana, “Je, mmemwona yule mtu aliyejitokeza? Ama kweli, amejitokeza kuwakejeli Waisraeli. Mfalme Shauli atampa mtu yeyote atakayemuua mtu huyo utajiri mwingi. Zaidi ya yote, atamwoza binti yake. Tena, watu wa jamaa ya baba yake watakuwa huru, hawatalipa kodi.”

26. Daudi akawauliza wale waliokuwa karibu naye, “Je, mtu atakayemuua Mfilisti huyu na kuikomboa Israeli kutokana na aibu hii atafanyiwa nini? Ni nani huyu Mfilisti, mtu asiyetahiriwa, anayethubutu kuyatukana majeshi ya Mungu aliye hai?”

27. Watu wakamwambia kama walivyokuwa wamesema hapo awali juu ya mtu atakayemuua Goliathi.

28. Lakini Eliabu, kaka mkubwa wa Daudi alipomsikia Daudi akiongea na watu, alimkasirikia Daudi, akasema, “Kwa nini umekuja? Je, wale kondoo wachache umemwachia nani kule nyikani? Najua ujeuri wako na uovu wako. Umekuja tu kutazama vita.”

29. Daudi akamjibu, “Sasa nimefanya nini? Je, siwezi kuuliza swali tu?”

30. Daudi akamgeukia mtu mwingine akamwuliza swali hilohilo; na kila alipouliza, alipata jibu lilelile.

31. Watu fulani ambao walimsikia Daudi alivyosema, walikwenda kumwambia Shauli. Naye Shauli akaagiza aitwe.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 17