Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 17:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Sasa, Wafilisti walikusanya majeshi yao huko Soko, mji ulioko katika Yuda, tayari kwa vita. Walipiga kambi katika sehemu moja iitwayo Efes-damimu kati ya Soko na Azeka.

2. Shauli pamoja na Waisraeli walikusanyika, na kupiga kambi katika bonde la Ela. Wakajipanga tayari kupigana na Wafilisti.

3. Wafilisti walisimama mlimani upande mmoja na Waisraeli walisimama mlimani upande mwingine, katikati yao kulikuwa na bonde.

4. Kutoka kwenye kambi ya Wafilisti, alijitokeza shujaa mmoja aitwaye Goliathi, mwenyeji wa mji wa Gathi. Urefu wake ulikaribia mita tatu.

5. Kichwani alivaa kofia ya shaba, na deraya ya shaba kifuani yenye uzito wa kilo 57.

6. Miguu yake pia ilikuwa na kinga ya shaba na mabegani pake alibeba mkuki wa shaba.

7. Mpini wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumanguo, na chembe cha mkuki huo, kilikuwa na uzito wa kilo saba. Ngao yake ilibebwa na mtu mwingine aliyemtangulia.

8. Goliathi alisimama na kuwapigia kelele wanajeshi wa Israeli, akisema, “Mnafanya nini hapo? Je, mmekuja kupigana vita? Mimi ni Mfilisti, nyinyi ni watumwa wa Shauli. Chagueni mtu mmoja wenu aje kupigana nami.

9. Akinishinda na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu. Lakini nikimshinda na kumuua basi, nyinyi mtakuwa watumwa wetu na kututumikia.”

10. Kisha Mfilisti huyo aliendelea kusema kwa majivuno, “Nawataka wanajeshi wa Israeli siku hii kumtoa mtu mmoja aje kupigana nami.”

11. Shauli pamoja na wanajeshi wote wa Israeli walipoyasikia maneno hayo ya Mfilisti huyo, walifadhaika na kuogopa sana.

12. Daudi alikuwa mtoto wa Yese, Mwefrathi kutoka Bethlehemu katika Yuda. Yese alikuwa na watoto wanane wa kiume. Wakati Shauli alipokuwa mfalme, yeye alikuwa tayari mzee, mtu mwenye umri mkubwa.

13. Wana wakubwa watatu wa Yese, Eliabu mzaliwa wa kwanza, Abinadabu aliyefuata na Shama wa tatu, walikuwa wamekwenda pamoja na Shauli vitani.

14. Daudi alikuwa ndiye mdogo wa wote. Wale watoto watatu wakubwa walikuwa wamekwenda na Shauli.

15. Ingawa Daudi mara kwa mara alikwenda kwa Shauli, alirudi nyumbani Bethlehemu kuchunga kondoo wa baba yake.

16. Kwa muda wa siku arubaini, asubuhi na jioni, yule Mfilisti Goliathi alijitokeza hadharani, akasimama na kuwakejeli wanajeshi wa Israeli.

17. Siku moja, Yese alimwambia mwanawe Daudi, “Wapelekee kaka zako bisi kilo kumi na mikate kumi. Wapelekee haraka huko kambini.

18. Na yule kamanda wao wa kikosi cha wanajeshi elfu mpelekee jibini hizi kumi. Kawaangalie kaka zako kama wanaendelea vizuri na kisha uniletee habari zao.”

Kusoma sura kamili 1 Samueli 17