Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 15:6-16 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Shauli akawaambia Wakeni, “Nendeni! Ondokeni! Tokeni miongoni mwa Waamaleki, la sivyo, nitawaangamiza pamoja nao. Ondokeni kwa sababu nyinyi mliwatendea wema Waisraeli walipotoka Misri.” Basi, Wakeni wakaondoka miongoni mwa Waamaleki.

7. Shauli aliwashinda Waamaleki kuanzia Havila hadi Shuri, mashariki ya Misri.

8. Alimteka mfalme Agagi wa Waamaleki akiwa hai. Akawaua watu kwa makali ya upanga.

9. Lakini Shauli na watu wake hawakumuua Agagi, wala kondoo bora kabisa, ng'ombe wazuri, ndama, wanakondoo na chochote kile kilichokuwa kizuri hawakukiangamiza. Lakini vitu vyote vibaya na visivyo na thamani waliviangamiza.

10. Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli,

11. “Ninajuta kwamba nimemfanya Shauli kuwa mfalme. Yeye ameacha kunifuata mimi na hajatimiza amri zangu.” Samueli alikasirika, akamlilia Mwenyezi-Mungu usiku kucha.

12. Samueli alisikia kuwa Shauli alikuwa amekuja huko Karmeli na amesimamisha mnara wa ukumbusho wake, na kwamba amekwenda Gilgali. Hivyo, kesho yake, Samueli aliamka asubuhi na mapema akaenda kukutana na Shauli.

13. Samueli alipomfikia Shauli, Shauli akamwambia Samueli, “Mwenyezi-Mungu na akubariki! Nimetekeleza amri ya Mwenyezi-Mungu.”

14. Samueli akamwambia, “Mbona nasikia mlio wa kondoo na ng'ombe?”

15. Shauli akajibu, “Watu waliwaacha hai kondoo na ng'ombe bora kabisa ili kumtambikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, lakini wengine wote tumewaangamiza.”

16. Samueli akamkatiza Shauli, “Nyamaza! Nitakuambia jambo aliloniambia Mwenyezi-Mungu leo usiku.” Shauli akasema, “Niambie.”

Kusoma sura kamili 1 Samueli 15