Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 14:42-52 Biblia Habari Njema (BHN)

42. Shauli akasema, “Pigeni kura kati yangu na mwanangu Yonathani.” Yonathani akapatikana kuwa na hatia.

43. Ndipo Shauli akamwambia Yonathani, “Niambie ulilofanya.” Yonathani akajibu, “Nilikula asali kidogo kwa kutumia fimbo yangu. Niko hapa na niko tayari kufa.”

44. Shauli akasema, “Mungu na anitendee mimi vivyo hivyo na hata na wengine. Yonathani ni lazima utauawa.”

45. Lakini watu wakamwambia Shauli, “Mbona Yonathani aliyeiletea Israeli ushindi huu mkubwa, auawe? Jambo hilo liwe mbali. Twaapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, hata unywele wa kichwa chake hautaanguka chini. Alichokifanya leo, amekifanya kwa msaada wa Mwenyezi-Mungu.” Hivyo, watu walimkomboa Yonathani naye hakuuawa.

46. Kisha Shauli aliacha kuwafuatia Wafilisti, nao Wafilisti wakarudi makwao.

47. Baada ya Shauli kuwa mfalme wa Israeli, alipigana na adui zake kila upande: Wamoabu, Waamoni, Waedomu, wafalme wa Soba, na Wafilisti. Kila alipopigana vita, alishinda.

48. Alipigana kwa uhodari, akawashinda Waamaleki. Aliwaokoa Waisraeli kutoka kwa watu wote waliowashambulia.

49. Watoto wa kiume wa Shauli walikuwa Yonathani, Ishvi na Malki-shua. Binti zake walikuwa wawili; mzaliwa wa kwanza aliitwa Merabu na mdogo aliitwa Mikali.

50. Mkewe Shauli aliitwa Ahinoamu binti Ahimaasi. Kamanda wa jeshi la Shauli aliitwa Abneri, mwana wa Neri, mjomba wa Shauli.

51. Baba wa Shauli alikuwa Kishi na baba wa Abneri alikuwa Neri mwana wa Abieli.

52. Kulikuwa na mapigano makali dhidi ya Wafilisti muda wote Shauli alipokuwa mfalme; na kila mara Shauli alipompata mtu mwenye nguvu au shujaa alimchukua ajiunge na jeshi.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 14