Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 14:13-24 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Basi, Yonathani akapanda kwa miguu na mikono, na yule kijana akamfuata. Yonathani aliwashambulia Wafilisti akiwaangusha chini huku yule kijana alifuata nyuma akiwaua.

14. Katika mashambulizi hayo ya kwanza Yonathani, akiwa pamoja na kijana wake aliyembebea silaha, aliwaua watu kama ishirini katika eneo la nchi lipatalo nusu eka.

15. Katika nchi nzima ya Wafilisti, wote walianza kufadhaika, wanajeshi kambini, watu mashambani, kwenye ngome, hata na washambuliaji walitetemeka; nchi ilitetemeka, na kulikuwa na woga mkubwa.

16. Wapelelezi wa Shauli huko Gibea katika nchi ya Benyamini waliwaona watu wengi wakikimbia huku na huko.

17. Shauli akawaambia watu waliokuwa pamoja naye, “Hebu jihesabuni ili kujua ni akina nani waliotutoroka.” Walipojihesabu, waligundua kuwa Yonathani na kijana aliyembebea silaha walikuwa hawapo.

18. Shauli akamwambia kuhani Ahiya, “Lilete hapa sanduku la Mungu.” (Wakati huo sanduku la agano la Mungu lilikuwa pamoja na Waisraeli.)

19. Shauli alipokuwa anaongea bado na kuhani, ghasia kambini kwa Wafilisti ziliongezeka zaidi na zaidi. Kwa hiyo Shauli akamwambia kuhani, “Acha; usililete tena sanduku la agano.”

20. Hivyo, Shauli na watu wake wakajipanga na kuingia vitani dhidi ya Wafilisti. Lakini Wafilisti walianza kushambuliana wenyewe kwa wenyewe kwa mvurugiko mkubwa.

21. Waebrania waliokuwa upande wa Wafilisti, na waliokwenda nao huko kambini, wakageuka na kujiunga na Waisraeli waliokuwa pamoja na Shauli na Yonathani.

22. Hata Waisraeli wengine waliokuwa wamejificha kwenye nchi ya milima ya Efraimu, waliposikia kuwa Wafilisti walikuwa wanakimbia, nao pia wakawafuatia na kuwapiga.

23. Hivyo Mwenyezi-Mungu aliwapa Waisraeli ushindi.Vita vilienea mpaka kupita Beth-aveni.

24. Siku ile, Waisraeli walisumbuliwa sana maana Shauli alikuwa amewaapisha watu, “Mtu yeyote atakayekula chakula kabla jua kutua, na kabla sijajilipiza kisasi cha adui zangu, na alaaniwe.” Hivyo, siku yote, hakuna mtu aliyeonja chakula chochote.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 14