Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 10:15-24 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Yule baba mdogo wa Shauli akamwambia, “Tafadhali, niambie kile alichokuambia Samueli.”

16. Shauli akajibu, “Alituambia waziwazi kuwa punda wamepatikana.” Lakini Shauli hakumweleza kuwa Samueli alimwambia kuwa atakuwa mfalme.

17. Samueli aliwaita watu wote wakusanyike mbele ya Mwenyezi-Mungu huko Mizpa.

18. Walipowasili aliwaambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anasema hivi: Niliwatoa Waisraeli nchini Misri, nikawaokoa nyinyi kutoka kwa Wamisri na falme nyingine zilizowakandamiza.

19. Lakini leo hii mmenikataa mimi Mungu wenu ambaye nawaokoa kutoka maafa na huzuni zenu; nanyi mmesema, ‘La! Tuwekee mfalme juu yetu.’ Sasa, basi, jikusanyeni nyote mbele yangu mkiwa katika makabila yenu na kwa maelfu yenu.”

20. Kisha Samueli akayapanga makabila yote ya Israeli, kabila la Benyamini likachukuliwa kwa kura.

21. Akalileta mbele kabila la Benyamini, kulingana na koo zake, na ukoo wa Matri ukachaguliwa kwa kura. Mwisho akauleta mbele ukoo wa Matri, na Shauli mwana wa Kishi akachaguliwa kwa kura. Lakini walipomtafuta hakupatikana.

22. Wakamwuliza Mungu tena, “Je, kuna mtu zaidi anayekuja?” Mwenyezi-Mungu akawajibu, “Anajificha kwenye mizigo.”

23. Basi, walikwenda mbio, wakamtafuta Shauli na kumleta. Shauli aliposimama miongoni mwa watu alikuwa mrefu kuliko watu wote, kuanzia mabegani.

24. Samueli akawaambia watu wote, “Huyu ndiye mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu katika watu wote; hakuna yeyote aliye kama yeye.” Watu wote wakapiga kelele: “Aishi mfalme.”

Kusoma sura kamili 1 Samueli 10