Agano la Kale

Agano Jipya

1 Mambo Ya Nyakati 29:11-22 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Ukuu ni wako, ee Mwenyezi-Mungu, una nguvu, utukufu, ushindi na enzi. Vyote vilivyoko mbinguni na duniani ni vyako. Ee Mwenyezi-Mungu, ufalme ni wako, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote.

12. Utajiri na heshima hutoka kwako, vyote wavitawala. Uwezo na nguvu vimo mkononi mwako, nawe wawakuza uwapendao, na huwaimarisha wote.

13. Sasa ee Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu jina lako tukufu.

14. “Lakini, mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kukupa kitu? Kwa maana vitu vyote vyatoka kwako, tumekutolea vilivyo vyako wewe mwenyewe.

15. Sisi tu wageni mbele yako, na wasafiri kama walivyokuwa babu zetu wote. Siku zetu duniani ni kama kivuli kipitacho, hapa hakuna tumaini la kukaa.

16. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wingi wote huu tuliotoa ili kukujengea nyumba kwa ajili ya utukufu wa jina lako takatifu, watoka mkononi mwako na yote ni yako.

17. Ninajua Mungu wangu, kwamba wewe waujaribu moyo, nawe unapendezwa na unyofu. Nami, katika unyofu wa moyo wangu nimetoa vitu hivi vyote kwa hiari yangu, na sasa ninaona watu wako walioko hapa, wakikutolea kwa hiari na furaha.

18. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Israeli, babu zetu, dumisha maazimio ya namna hiyo na fikira za namna hiyo mioyoni mwa watu wako, na ielekeze mioyo ya watu wako kwako.

19. Mjalie Solomoni mwanangu ili kwa moyo wote ashike amri zako, maamuzi na maagizo yako, atekeleze yote ili aweze kuijenga nyumba hii ya enzi niliyoifanyia matayarisho.”

20. Kisha, mfalme Daudi aliwaambia wote waliokusanyika, “Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Na wote waliokusanyika wakamtukuza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, wakamsujudia na kumwabudu Mwenyezi-Mungu na kumtolea mfalme Daudi heshima.

21. Wakamtolea tambiko Mwenyezi-Mungu. Siku ya pili yake wakamtolea sadaka za kuteketezwa: Mafahali 1,000, wanakondoo 1,000, pamoja na sadaka zao za vinywaji na tambiko nyingi kwa ajili ya Waisraeli wote.

22. Basi siku hiyo walikula na kunywa kwa furaha kuu mbele ya Mwenyezi-Mungu.Wakamtawaza Solomoni mwana wa Daudi, mara ya pili. Wakampaka mafuta awe mtawala kwa jina la Mwenyezi-Mungu, na Sadoki awe kuhani.

Kusoma sura kamili 1 Mambo Ya Nyakati 29