Agano la Kale

Agano Jipya

1 Mambo Ya Nyakati 22:7-19 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Daudi akamwambia Solomoni, “Mwanangu, nilikusudia moyoni mwangu kumjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu nyumba ili kumtukuza.

8. Lakini Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Wewe umemwaga damu nyingi kwa kupigana vita vikubwa. Kwa sababu ya damu nyingi ambayo umemwaga mbele yangu hapa duniani, hutanijengea nyumba.

9. Hata hivyo, utapata mwana, ambaye atatawala kwa amani kwa sababu nitampa amani na maadui zake wote wa jirani. Jina lake litakuwa Solomoni, kwa maana katika siku za utawala wake, atailetea Israeli amani na utulivu.

10. Hivyo, yeye ndiye atakayenijengea nyumba. Atakuwa mwanangu nami nitakuwa baba yake, na wazawa wake wataitawala Israeli milele.’

11. Sasa mwanangu, Mwenyezi-Mungu, Mungu wako na awe pamoja nawe ili ufaulu kumjengea nyumba kama alivyosema.

12. Mwenyezi-Mungu akupe busara na akili ili atakapokupa uongozi juu ya Israeli, uzishike sheria zake Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.

13. Ukiwa mwangalifu, na ukizitii amri ambazo Mwenyezi-Mungu alimwagiza Mose juu ya Israeli, utastawi. Jipe moyo, uwe imara. Usiogope wala usifadhaike.

14. Kwa juhudi kubwa, nimeiwekea akiba nyumba ya Mwenyezi-Mungu, talanta 100,000 za dhahabu, talanta 1,000,000 za fedha na idadi isiyopimika ya shaba na chuma, kwani ni nyingi sana. Nimeandaa mbao na mawe tayari. Lakini huna budi kuongezea.

15. Unao wafanyakazi wengi: Kuna wachonga mawe, waashi, maseremala na mafundi wa kila aina wenye ujuzi mwingi;

16. wa kufua dhahabu, fedha, shaba na chuma. Haya! Anza kazi! Mwenyezi-Mungu na awe pamoja nawe!”

17. Zaidi ya hayo, Daudi aliwaamuru viongozi wote wa Waisraeli wamsaidie Solomoni mwanawe, akisema,

18. “Je, Mwenyezi-Mungu Mungu wenu hayuko pamoja nanyi? Je, hajawapa amani katika pande zote? Yeye aliwatia wakazi wa nchi hii mikononi mwangu na sasa wako chini ya Mwenyezi-Mungu na watu wake.

19. Sasa, mtumikieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa nia na moyo wote. Shime basi! Mjengeeni Mwenyezi-Mungu mahali patakatifu ili sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu pamoja na vyombo vyote vitakatifu vitumiwavyo katika ibada, viwekwe ndani ya nyumba iliyojengwa kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu.”

Kusoma sura kamili 1 Mambo Ya Nyakati 22