Agano la Kale

Agano Jipya

1 Mambo Ya Nyakati 11:14-31 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Lakini Daudi na Eliazari walisimama imara katikati ya shamba hilo ili kulitetea, wakawaua Wafilisti; Mwenyezi-Mungu akawaokoa kwa kuwapa ushindi mkubwa.

15. Kisha mashujaa watatu kati ya wakuu thelathini waliteremka hadi kwenye mwamba, wakamwendea Daudi kwenye pango huko Adulamu. Wakati huo jeshi la Wafilisti lilikuwa limepiga kambi katika bonde la Refaimu.

16. Naye Daudi wakati huo alikuwa katika ngome, nalo jeshi la Wafilisti lilikuwa mjini Bethlehemu.

17. Daudi akasema kwa hamu kubwa, “Laiti kama mtu angeweza kunipa maji ya kunywa kutoka katika kisima cha Bethlehemu kilicho karibu na lango la mji!”

18. Wale mashujaa wake watatu walitoka, wakapenya katikati ya kambi ya jeshi la Wafilisti, wakaenda na kuchota maji katika kisima cha Bethlehemu, karibu na lango la mji, wakamletea Daudi. Lakini Daudi akakataa kuyanywa, na badala yake akayamwaga chini kama tambiko kwa Mwenyezi-Mungu

19. akisema, “Tendo kama hili lipitishie mbali nami; siwezi kulifanya mbele ya Mungu wangu. Je, waweza kunywa damu ya maisha ya watu hawa? Maana kwa kuyahatarisha maisha yao walileta maji haya.” Kwa hiyo Daudi hakuyanywa maji hayo. Hayo ndio mambo waliyotenda wale mashujaa watatu.

20. Abishai, nduguye Yoabu, alikuwa mkuu wa mashujaa thelathini. Yeye alipigana kwa mkuki wake dhidi ya watu 300, akawaua, akajipatia jina miongoni mwa wale mashujaa watatu.

21. Basi, akawa mashuhuri zaidi miongoni mwa mashujaa thelathini, hata akawa kamanda wao, lakini hakuwa shujaa kama wale mashujaa watatu.

22. Naye Benaya, mwana wa Yehoyada, kutoka Kabzeeli, alikuwa askari shujaa ambaye alifanya mambo mengi ya ajabu. Aliwaua mashujaa wawili kutoka Moabu, na siku moja wakati wa barafu, alishuka na kuua simba shimoni.

23. Vilevile, alimuua Mmisri mmoja, mtu mrefu sana, urefu wake kama mita mbili, naye mkononi mwake alikuwa amebeba mkuki mkubwa sana, kama mti wa mfumaji. Lakini Benaya alimwendea akiwa na fimbo tu, akamnyanganya mkuki huo, na kumuua Mmisri huyo kwa mkuki wake mwenyewe.

24. Benaya, mwana wa Yehoyada alifanya mambo haya, akajipatia jina miongoni mwa wale mashujaa watatu.

25. Basi, akawa mashuhuri kati ya wale mashujaa thelathini, ingawa hakuwa shujaa kama wale mashujaa watatu. Na Daudi akampa cheo cha mkuu wa walinzi wake binafsi.

26. Wanajeshi mashujaa wa Daudi walikuwa: Asaheli nduguye Yoabu, Elhanani mwana wa Dodo wa Bethlehemu,

27. Shamothi Mharodi, Helesi Mpeloni,

28. Ira, mwana wa Ikeshi Mtekoa, Abiezeri Mwanathothi;

29. Sibekai Mhushathi; Ilai Mwahohi;

30. Maharai Mnetofathi; Heledi, mwana wa Baana Mnetofathi;

31. Itai, mwana wa Ribai, kutoka Gibea, wa kabila la Benyamini; Benaya Mpirathoni;

Kusoma sura kamili 1 Mambo Ya Nyakati 11