Agano la Kale

Agano Jipya

Waroma 6:7-18 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Kwa maana, mtu aliyekufa, amenasuliwa kutoka dhambini.

8. Basi, ikiwa tumekufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba tutaishi pia pamoja naye.

9. Maana, tunajua kwamba Kristo amekwisha fufuliwa kutoka kwa wafu na hafi tena; kifo hakimtawali tena.

10. Hivyo, kwa kuwa alikufa – mara moja tu – dhambi haina nguvu tena juu yake; na sasa anaishi maisha yake katika umoja na Mungu.

11. Hali kadhalika nanyi lazima mjione kuwa mmekufa kuhusu dhambi, lakini kama mnaoishi katika umoja na Mungu kwa njia ya Kristo Yesu.

12. Kwa hiyo, dhambi isiitawale tena miili yenu ambayo hufa, na hivyo kuzitii tamaa zake.

13. Wala msitoe hata sehemu moja ya miili yenu iwe chombo cha kutenda uovu na dhambi. Badala yake, jitoleeni nyinyi wenyewe kwa Mungu kama watu waliofufuliwa kutoka kwa wafu; toeni nafsi zenu zote kwa Mungu kwa ajili ya uadilifu.

14. Maana, dhambi haitawatawala tena, kwani hamko chini ya sheria, bali chini ya neema.

15. Basi, tuseme nini? Je, tutende dhambi ati kwa sababu hatuko chini ya sheria bali chini ya neema? Hata kidogo!

16. Mnajua kwamba mkijitolea nyinyi wenyewe kama watumwa na kumtii fulani, mnakuwa kweli watumwa wake mtu huyo – au watumwa wa dhambi na matokeo yake ni kifo, au wa utii na matokeo yake ni kufanywa kuwa waadilifu.

17. Ingawa mlikuwa watumwa wa dhambi zamani, sasa lakini – namshukuru Mungu – mmetii kwa moyo wote yale maazimio na mafundisho mliyopokea.

18. Mlikombolewa kutoka utumwa wa dhambi, mkawa watumwa wa uadilifu

Kusoma sura kamili Waroma 6