Agano la Kale

Agano Jipya

Waroma 6:13-23 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Wala msitoe hata sehemu moja ya miili yenu iwe chombo cha kutenda uovu na dhambi. Badala yake, jitoleeni nyinyi wenyewe kwa Mungu kama watu waliofufuliwa kutoka kwa wafu; toeni nafsi zenu zote kwa Mungu kwa ajili ya uadilifu.

14. Maana, dhambi haitawatawala tena, kwani hamko chini ya sheria, bali chini ya neema.

15. Basi, tuseme nini? Je, tutende dhambi ati kwa sababu hatuko chini ya sheria bali chini ya neema? Hata kidogo!

16. Mnajua kwamba mkijitolea nyinyi wenyewe kama watumwa na kumtii fulani, mnakuwa kweli watumwa wake mtu huyo – au watumwa wa dhambi na matokeo yake ni kifo, au wa utii na matokeo yake ni kufanywa kuwa waadilifu.

17. Ingawa mlikuwa watumwa wa dhambi zamani, sasa lakini – namshukuru Mungu – mmetii kwa moyo wote yale maazimio na mafundisho mliyopokea.

18. Mlikombolewa kutoka utumwa wa dhambi, mkawa watumwa wa uadilifu

19. (hapa natumia lugha ya kawaida ya watu kwa sababu ya udhaifu wenu wenyewe). Kama vile wakati fulani mlivyojitolea nyinyi wenyewe kutumikia uchafu na uhalifu kwa ajili ya uovu, vivyo hivyo sasa jitoleeni nafsi zenu wenyewe kutumikia uadilifu kwa ajili ya utakatifu.

20. Mlipokuwa watumwa wa dhambi mlikuwa huru mbali na uadilifu.

21. Sasa, mlipata faida gani siku zile kutokana na mambo yale ambayo mnayaonea aibu sasa? Maana, matokeo ya mambo haya ni kifo!

22. Lakini sasa mmekwisha kombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mmekuwa watumishi wa Mungu; faida mliyo nayo sasa ni utakatifu, na matokeo yake ni uhai wa milele.

23. Kwa maana mshahara wa dhambi ni kifo; lakini zawadi anayotoa Mungu ni uhai wa milele katika kuungana na Kristo Yesu, Bwana wetu.

Kusoma sura kamili Waroma 6