Agano la Kale

Agano Jipya

Waroma 12:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Kwa hiyo, ndugu zangu, maadamu Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: Mtoleeni Mungu miili yenu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye kupendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu.

2. Msiige mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza fikira zenu. Hapo ndipo mtakapoweza kuyajua mapenzi ya Mungu na kutambua jambo lililo jema, linalompendeza na kamilifu.

3. Kutokana na neema aliyonijalia Mungu, nawaambieni nyinyi nyote: Msijione kuwa ni kitu zaidi kuliko mnavyopaswa kuwa. Fikira zenu na ziwe na kiasi kadiri ya kipimo cha imani Mungu aliyomgawia kila mmoja.

4. Mwili una viungo vingi, kila kimoja na kazi yake.

5. Hali kadhalika ingawa sisi ni wengi, tu mwili mmoja kwa kuungana na Kristo, na kila mmoja ni kiungo cha mwenzake.

6. Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kadiri ya neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha unabii na akitumie kadiri ya imani yake.

7. Mwenye kipaji cha utumishi na atumikie. Mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe.

8. Mwenye kipaji cha kuwafariji wengine na afanye hivyo. Mwenye kumgawia mwenzake alicho nacho na afanye hivyo kwa ukarimu. Msimamizi na asimamie kwa bidii; naye mwenye kutenda jambo la huruma na afanye hivyo kwa furaha.

9. Mapendo yenu na yawe bila unafiki wowote. Chukieni jambo lolote ovu, zingatieni jema.

10. Pendaneni kindugu; kila mmoja amfikirie kwanza mwenzake kwa heshima.

11. Msilegee katika bidii, ila muwe wachangamfu rohoni katika kumtumikia Bwana.

Kusoma sura kamili Waroma 12