Agano la Kale

Agano Jipya

Wakolosai 1:10-28 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Hapo mtaweza kuishi kama anavyotaka Bwana na kutenda daima yanayompendeza. Maisha yenu yatakuwa yenye matunda ya kila namna ya matendo mema na mtazidi kukua katika kumjua Mungu.

11. Mungu awajalieni nguvu kwa uwezo wake mtukufu ili muweze kustahimili kila kitu kwa uvumilivu.

12. Na kwa furaha mshukuruni Baba, aliyewawezesha nyinyi kuwa na sehemu yenu katika mambo yale aliyowawekea watu wake katika ufalme wa mwanga.

13. Yeye alituokoa katika nguvu ya giza, akatuleta salama katika ufalme wa Mwanae mpenzi.

14. Kwake yeye tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa.

15. Kristo ni mfano wa Mungu asiyeonekana;ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.

16. Maana kwake vitu vyote viliumbwakila kitu duniani na mbinguni,vitu vinavyoonekana na visivyoonekana:Wenye enzi, watawala, wakuu na wenye nguvu.Vyote viliumbwa kwake na kwa ajili yake.

17. Yeye alikuwako kabla ya vitu vyote;vyote huendelea kuwako kwa uwezo wake.

18. Yeye ni kichwa cha mwili wake, yaani kanisa;yeye ni chanzo cha uhai wa huo mwili.Yeye ndiye mwanzo,mzaliwa wa kwanza aliyefufuliwa kutoka kwa wafu,ili awe na nafasi ya kwanza katika vitu vyote.

19. Maana Mungu alipenda utimilifu wake wote uwe ndani yake.

20. Kwake vitu vyote vilipatanishwa na Mungu:Na kwa damu yake msalabani akafanya amanina vitu vyote duniani na mbinguni.

21. Hapo kwanza nyinyi pia mlikuwa mbali na Mungu na mlikuwa maadui zake kwa sababu ya fikira zenu na matendo yenu maovu.

22. Lakini sasa, kwa kifo cha Mwanae aliyeishi hapa duniani, Mungu amewapatanisha naye, kusudi awaweke mbele yake mkiwa watakatifu, safi na bila lawama.

23. Mnapaswa, lakini kuendelea na msingi imara katika imani, wala msikubali kutikiswa kutoka katika tumaini lile mlilopata wakati mlipoisikia Injili. Mimi Paulo nimekuwa mtumishi wa hiyo Injili ambayo imekwisha hubiriwa kila mtu duniani.

24. Na sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa mateso yangu hapa duniani, nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, yaani kanisa.

25. Nami nimefanywa kuwa mtumishi wa kanisa kufuatana na mpango wake Mungu ambao alinikabidhi kwa faida yenu. Mpango wenyewe ni kuutangaza kwa ukamilifu ujumbe wake,

26. ambao ni siri aliyowaficha binadamu wote tangu milele, lakini sasa amewajulisha watu wake.

27. Mungu ametaka kuwajulisha hao jinsi siri hiyo ilivyo kuu na tukufu ambayo imeenea kwa watu wa mataifa, nayo ndiyo hii: Kristo yuko ndani yenu, na jambo hilo lamaanisha kwamba nyinyi mtaushiriki utukufu wa Mungu.

28. Kwa sababu hiyo tunamhubiri Kristo kwa watu wote; tunawaonya na kuwafundisha wote kwa hekima yote, ili tuweze kumleta kila mmoja mbele ya Mungu akiwa amekomaa katika kuungana na Kristo.

Kusoma sura kamili Wakolosai 1