Agano la Kale

Agano Jipya

Wagalatia 4:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Basi, nasema hivi: Mrithi, akiwa bado mtoto, hawi tofauti na mtumwa ingawaje mali yote ni yake.

2. Wakati huo wote yuko chini ya walezi na wadhamini mpaka wakati ule uliowekwa na baba yake.

3. Hali kadhalika na sisi tulipokuwa bado watoto, tulikuwa watumwa wa pepo watawala wa ulimwengu.

4. Lakini wakati ule maalumu ulipotimia, Mungu alimtuma Mwanae aliyezaliwa na mwanamke, akaishi chini ya sheria,

5. apate kuwakomboa wale waliokuwa chini ya sheria ili sisi tufanywe wana wa Mungu.

6. Kwa vile sasa nyinyi ni wanawe, Mungu amemtuma Roho wa Mwanae mioyoni mwenu, Roho ambaye hulia “Aba,” yaani “Baba.”

7. Basi, wewe si mtumwa tena, bali mwana. Na ikiwa ni mwana, basi, wewe utapokea yote Mungu aliyowawekea watoto wake.

8. Zamani hamkumjua Mungu na hivyo mliitumikia miungu isiyo miungu kweli.

9. Lakini sasa, kwa vile mnamjua Mungu, au tuseme mnajulikana na Mungu, mnawezaje tena kurudi kwa wale pepo maskini na dhaifu hata kutaka kuwatumikia tena?

10. Bado mnaadhimisha siku, miezi na miaka!

11. Nahofu kwamba labda kazi niliyoifanya kwa ajili yenu imepotea bure!

12. Ndugu, nawasihi muwe kama mimi, kwa vile hata mimi nimekuwa kama nyinyi. Hamkunitendea ubaya wowote.

13. Mnajua kwamba ugonjwa wangu ndio ulionipatia fursa ya kuwahubirieni Injili kwa mara ya kwanza.

14. Hata hivyo, wakati ule hamkunidharau wala kunikataa kwa sababu ya udhaifu wangu ingawa mlishawishiwa kufanya hivyo; lakini mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama vile ningekuwa Kristo Yesu mwenyewe.

15. Mlikuwa wenye furaha; sasa kumetokea nini? Naapa kwamba wakati ule mngaliweza hata kuyangoa macho yenu na kunipa mimi.

Kusoma sura kamili Wagalatia 4