Agano la Kale

Agano Jipya

Wagalatia 3:16-23 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Basi, Abrahamu alipewa ahadi, yeye pamoja na mzawa wake. Maandiko hayasemi: “Na wazawa wake,” yaani wengi, bali yasema, “Na mzawa wake,” yaani mmoja, naye ndiye Kristo.

17. Ninachotaka kusema ni hiki: Mungu alifanya agano lake, akalithibitisha; sheria ambayo ilitokea miaka 430 baadaye, haiwezi kulitangua hilo agano wala kuibatilisha hiyo ahadi.

18. Maana, kama zawadi ya Mungu inategemea sheria, basi, haiwezi kutegemea tena ahadi ya Mungu. Kumbe, lakini Mungu alimkirimia Abrahamu kwa sababu aliahidi.

19. Ya nini basi, sheria? Iliongezwa hapo ili kuonesha uhalifu ni kitu gani, mpaka atakapokuja yule mzawa wa Abrahamu aliyepewa ile ahadi. Sheria ililetwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi.

20. Ama hakika, mpatanishi hahitajiwi ikiwa jambo lenyewe lamhusu mtu mmoja; na Mungu ni mmoja.

21. Je, sheria inapingana na ahadi za Mungu? Hata kidogo! Maana, kama kungalitolewa sheria ambayo ingeweza kuwapa watu uhai, basi, tungeweza kufanywa waadilifu kwa njia ya sheria.

22. Lakini sivyo; Maandiko Matakatifu yamekwisha sema kwamba ulimwengu wote upo chini ya utawala wa dhambi; na hivyo, wenye kuamini watimiziwe ile ahadi aliyotoa Mungu, kwa kumwamini Yesu Kristo.

23. Kabla ya kujaliwa imani, sheria ilitufanya wafungwa, tukingojea imani hiyo ifunuliwe.

Kusoma sura kamili Wagalatia 3