Agano la Kale

Agano Jipya

Wagalatia 2:3-16 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Lakini, hata mwenzangu Tito, ambaye ni Mgiriki, hakulazimika kutahiriwa,

4. ingawa kulikuwa na ndugu wengine wa uongo waliotaka atahiriwe. Watu hawa walijiingiza kwa ujanja na kupeleleza uhuru wetu tulio nao katika kuungana na Kristo Yesu, ili wapate kutufanya watumwa.

5. Hatukukubaliana nao hata kidogo ili ukweli wa Injili ubaki nanyi daima.

6. Lakini watu hawa wanaosemekana kuwa ni viongozi – kama kweli walikuwa hivyo au sivyo, kwangu si kitu, maana Mungu hahukumu kwa kuangalia mambo ya nje – watu hawa hawakuwa na mawazo ya kuniongezea.

7. Badala yake, walitambua kwamba Mungu alikuwa amenituma kuhubiri Injili kwa watu wa mataifa mengine kama vile Petro alivyokuwa ametumwa kuihubiri kwa Wayahudi.

8. Maana, yule aliyemwezesha Petro kuwa mtume kwa Wayahudi, ndiye aliyeniwezesha nami pia kuwa mtume kwa watu wa mataifa mengine.

9. Basi, Yakobo, Kefa na Yohane, ambao waonekana kuwa viongozi wakuu, walitambua kwamba Mungu alinijalia neema hiyo, wakatushika sisi mkono, yaani Barnaba na mimi, iwe ishara ya ushirikiano. Sisi ilitupasa tukafanye kazi kati ya watu wa mataifa mengine, na wao kati ya Wayahudi.

10. Wakatuomba lakini kitu kimoja: Tuwakumbuke maskini; jambo ambalo nimekuwa nikijitahidi kutekeleza.

11. Lakini Kefa alipofika Antiokia nilimpinga waziwazi maana alikuwa amekosea.

12. Awali, kabla ya watu kadhaa waliokuwa wametumwa na Yakobo kuwasili hapo, Petro alikuwa akila pamoja na watu wa mataifa mengine. Lakini, baada ya hao watu kufika, aliacha kabisa kula pamoja na watu wa mataifa mengine, kwa kuogopa kikundi cha waliosisitiza tohara.

13. Hata ndugu wengine Wayahudi walimuunga mkono Petro katika kitendo hiki cha unafiki, naye Barnaba akakumbwa na huo unafiki wao.

14. Basi, nilipoona kuwa msimamo wao kuhusu ukweli wa Injili haukuwa umenyooka, nikamwambia Kefa mbele ya watu wote: “Ingawa wewe ni Myahudi, unaishi kama watu wa mataifa mengine na si kama Myahudi! Unawezaje, basi kujaribu kuwalazimisha watu wa mataifa mengine kuishi kama Wayahudi?”

15. Kweli, sisi kwa asili ni Wayahudi, na si watu wa mataifa mengine wenye dhambi!

16. Lakini, tunajua kwa hakika kwamba mtu hawezi kufanywa mwadilifu kwa kuitii sheria, bali tu kwa kumwamini Yesu Kristo. Na sisi pia tumemwamini Yesu Kristo ili tupate kufanywa waadilifu kwa njia ya imani yetu kwa Kristo, na si kwa kuitii sheria.

Kusoma sura kamili Wagalatia 2