Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 5:18-29 Biblia Habari Njema (BHN)

18. Kweli nawaambieni, mpaka hapo mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata nukta moja au sehemu ndogo kabisa ya sheria itakayoondolewa, mpaka yote yametimia.

19. Basi, yeyote atakayevunja hata amri moja ndogo kuliko zote, na kuwafundisha wengine wafanye hivyo, huyo atakuwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni. Lakini yule atakayezishika na kuwafundisha wengine, huyo atakuwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.

20. Ndio maana nawaambieni, wema wenu usipozidi ule wa waalimu wa sheria na wa Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.

21. “Mmekwisha sikia ya kuwa watu wa kale waliambiwa: ‘Usiue! Atakayeua lazima ahukumiwe.’

22. Lakini mimi nawaambieni, yeyote anayemkasirikia ndugu yake, lazima ahukumiwe. Anayemdharau ndugu yake atapelekwa mahakamani. Anayemwita ndugu yake: ‘Pumbavu’ atastahili kuingia katika moto wa Jehanamu.

23. “Basi, ukipeleka sadaka yako mbele ya madhabahu na hapo ukakumbuka kwamba ndugu yako ana ugomvi nawe,

24. iache sadaka yako mbele ya madhabahu, nenda kwanza ukapatane na ndugu yako, ndipo urudi utoe sadaka yako.

25. “Patana na mshtaki wako upesi mkiwa bado njiani kwenda mahakamani. La sivyo, mshtaki wako atakukabidhi kwa hakimu, naye hakimu atakukabidhi kwa askari, nawe utafungwa gerezani.

26. Kweli nakuambia, hutatoka humo mpaka umelipa senti ya mwisho.

27. “Mmesikia kwamba watu waliambiwa: ‘Usizini!’

28. Lakini mimi nawaambieni, atakayemtazama mwanamke kwa kumtamani, amekwisha zini naye moyoni mwake.

29. Basi, kama jicho lako la kulia linakukosesha, lingoe ukalitupe mbali. Afadhali zaidi kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako, kuliko mwili wako wote kutupwa katika moto wa Jehanamu.

Kusoma sura kamili Mathayo 5