Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 27:22-34 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Pilato akawauliza, “Sasa, nifanye nini na Yesu aitwaye Kristo?” Wote wakasema, “Asulubiwe!”

23. Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya ubaya gani?” Wao wakazidi kupaza sauti: “Asulubiwe!”

24. Basi, Pilato alipotambua kwamba hafanikiwi chochote na kwamba maasi yalikuwa yanaanza, alichukua maji, akanawa mikono mbele ya ule umati wa watu, akasema, “Mimi sina lawama juu ya kifo cha mtu huyu; shauri lenu wenyewe.”

25. Watu wote wakasema, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!”

26. Hapo Pilato akawafungulia Baraba kutoka gerezani, na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa asulubiwe.

27. Kisha askari wa mkuu wa mkoa wakamwingiza Yesu ndani ya ikulu, wakamkusanyikia kikosi kizima.

28. Wakamvua nguo zake, wakamvika joho la rangi nyekundu.

29. Kisha wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani, wakamwekea pia mwanzi katika mkono wake wa kulia. Wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki wakisema, “Shikamoo mfalme wa Wayahudi!”

30. Wakamtemea mate, wakauchukua ule mwanzi, wakampiga nao kichwani.

31. Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha.

32. Walipokuwa wakienda, wakamkuta mtu mmoja jina lake Simoni, mwenyeji wa Kurene, wakamlazimisha kuuchukua msalaba wake Yesu.

33. Walipofika mahali paitwapo Golgotha, maana yake, mahali pa Fuvu la Kichwa,

34. wakampa mchanganyiko wa divai na kitu kichungu. Lakini Yesu alipoonja akakataa kunywa.

Kusoma sura kamili Mathayo 27