Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 21:23-35 Biblia Habari Njema (BHN)

23. Yesu aliingia hekaluni, akawa anafundisha. Alipokuwa akifundisha, makuhani wakuu na wazee wa watu wakamwuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Nani amekupa mamlaka haya?”

24. Yesu akawajibu, “Na mimi nitawaulizeni swali moja; mkinijibu, basi nami nitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.

25. Je, mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka kwa nani? Je, yalitoka mbinguni ama kwa watu?” Lakini wakajadiliana wao kwa wao hivi: “Tukisema, ‘Yalitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Basi, mbona hamkumsadiki?’

26. Na tukisema, ‘Yalitoka kwa watu,’ tunaogopa umati wa watu maana wote wanakubali kwamba Yohane ni nabii.”

27. Basi, wakamjibu, “Hatujui!” Naye Yesu akawaambia, “Nami pia sitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.

28. “Nyinyi mnaonaje; mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwambia yule wa kwanza, ‘Mwanangu, leo nenda ukafanye kazi katika shamba la mizabibu.’

29. Yule kijana akamwambia, ‘Sitaki!’ Lakini baadaye akabadili nia, akaenda kufanya kazi.

30. Yule baba akamwambia mtoto wake wa pili vivyo hivyo, naye akamjibu, ‘Naam baba!’ Lakini hakuenda kazini.

31. Je, ni nani kati ya hawa wawili aliyetimiza matakwa ya baba yake?” Wakamjibu, “Yule mtoto wa kwanza.”Basi, Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, watozaushuru na waasherati wataingia katika ufalme wa Mungu kabla yenu.

32. Maana Yohane alikuja kwenu akawaonesha njia adili ya kuishi, nanyi hamkumwamini; lakini watozaushuru na waasherati walimwamini. Hata baada ya kuona hayo yote nyinyi hamkutubu na kumsadiki.”

33. Yesu akasema, “Sikilizeni mfano mwingine. Mtu mmoja mwenye nyumba alilima shamba la mizabibu; akalizungushia ukuta, akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga humo mnara pia. Kisha akalikodisha kwa wakulima, akasafiri kwenda hadi nchi ya mbali.

34. Wakati wa mavuno ulipofika, aliwatuma watumishi wake kwa wale wakulima, ili wakachukue sehemu ya mavuno yake.

35. Wale wakulima wakawakamata hao watumishi; mmoja wakampiga, mwingine wakamuua na mwingine wakampiga mawe.

Kusoma sura kamili Mathayo 21