Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 16:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mafarisayo na Masadukayo walimwendea Yesu, na kwa kumjaribu, wakamwomba awaoneshe ishara kutoka mbinguni.

2. Lakini Yesu akawajibu, [“Ikifika jioni nyinyi husema: ‘Hali ya hewa itakuwa nzuri kwa maana anga ni jekundu!’

3. Na alfajiri mwasema: ‘Leo hali ya hewa itakuwa ya dhoruba, maana anga ni jekundu na tena mawingu yametanda!’ Basi, nyinyi mnajua sana kusoma majira kwa kuangalia hali ya anga, lakini kutambua dalili za nyakati hizi hamjui.]

4. Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Kinataka ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ishara ile ya Yona.” Basi, akawaacha, akaenda zake.

5. Wanafunzi wake walipokwisha vukia upande wa pili wa ziwa, walijikuta wamesahau kuchukua mikate.

6. Yesu akawaambia, “Muwe macho na mjihadhari na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!”

7. Lakini wao wakawa wanajadiliana: “Anasema hivyo kwa kuwa hatukuchukua mikate.”

8. Yesu alijua mawazo yao, akawaambia, “Enyi watu wenye imani haba! Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate?

9. Je, hamjaelewa bado? Je, hamkumbuki nilipoimega ile mikate mitano kwa ajili ya wale watu 5,000? Je, mlijaza vikapu vingapi vya mabaki?

10. Au, ile mikate saba waliyogawiwa wale watu 4,000, je, mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki.

11. Mbona hamwelewi ya kwamba sikuwa nikisema juu ya mikate? Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!”

12. Hapo wanafunzi wakafahamu kwamba aliwaambia wajihadhari siyo na chachu ya mikate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.

Kusoma sura kamili Mathayo 16