Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 15:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Kisha Mafarisayo na waalimu wa sheria wakafika kutoka Yerusalemu, wakamwendea Yesu, wakamwuliza,

2. “Kwa nini wanafunzi wako hawajali mapokeo tuliyopokea kwa wazee wetu? Hawanawi mikono ipasavyo kabla ya kula!”

3. Yesu akawajibu, “Kwa nini nanyi hamjali sheria ya Mungu ila mnapendelea mapokeo yenu wenyewe?

4. Mungu amesema: ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na ‘Anayemtukana baba yake au mama yake, lazima auawe.’

5. Lakini nyinyi mwafundisha ati mtu akiwa na kitu ambacho angeweza kumsaidia nacho baba yake au mama yake, lakini akasema: ‘Kitu hiki nimemtolea Mungu,’

6. basi, hapaswi tena kumheshimu baba yake! Ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa kufuata mafundisho yenu wenyewe.

7. Enyi wanafiki! Isaya alitabiri sawa kabisa juu yenu:

8. ‘Mungu asema: Watu hawa huniheshimu kwa maneno tu,lakini mioyoni mwao wako mbali nami.

9. Kuniabudu kwao hakufai,maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.’”

Kusoma sura kamili Mathayo 15