Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 8:7-26 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Maana pepo wachafu waliokuwa wamewapagaa watu wengi waliwatoka wakipiga kelele kubwa; na pia watu wengi waliokuwa wamepooza viungo na waliolemaa waliponywa.

8. Kukawa na furaha kubwa katika mji ule.

9. Basi, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Simoni ambaye alikuwa amekwisha fanya uchawi wake katika mji huo kwa muda na kuwashangaza watu wa Samaria, akijiona kuwa yeye ni mtu maarufu.

10. Watu wote, wadogo kwa wakubwa, walimsikiliza kwa makini wakisema, “Simoni ndiye nguvu ya kimungu inayoitwa ‘Nguvu Kubwa.’”

11. Walivutiwa sana naye kwa vile alikuwa amewashangaza kwa uchawi wake kwa muda mrefu.

12. Lakini walipouamini ujumbe wa Filipo juu ya Habari Njema ya ufalme wa Mungu na jina la Yesu Kristo, walibatizwa, wanawake na wanaume.

13. Hata Simoni aliamini; na baada ya kubatizwa alikuwa akiandamana na Filipo, akastaajabia maajabu na miujiza iliyokuwa inafanyika.

14. Wale mitume waliokuwa kule Yerusalemu walipopata habari kwamba wenyeji wa Samaria nao wamelipokea neno la Mungu, waliwatuma huko Petro na Yohane.

15. Walipofika waliwaombea hao waumini ili wampokee Roho Mtakatifu;

16. maana wakati huo Roho Mtakatifu hakuwa amemshukia yeyote kati yao; walikuwa wamebatizwa tu kwa jina la Bwana Yesu.

17. Basi, Petro na Yohane wakawawekea mikono hao waumini, nao wakampokea Roho Mtakatifu.

18. Hapo Simoni alingamua kwamba kwa kuwekewa mikono ya mitume waumini walipewa Roho Mtakatifu. Hivyo aliwapa Petro na Yohane fedha akisema,

19. “Nipeni na mimi uwezo huo ili yeyote nitakayemwekea mikono, apokee Roho Mtakatifu.”

20. Lakini Petro akamjibu, “Potelea mbali na fedha zako kwa vile unafikiri kwamba unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha!

21. Huna sehemu yoyote wala haki katika kazi hiyo kwa maana moyo wako hauko sawa mbele ya macho ya Mungu.

22. Kwa hiyo, tubu ubaya wako huu na umwombe Bwana naye anaweza kukusamehe fikira kama hizo.

23. Ni dhahiri kwangu kwamba umejaa wivu mkali na u mfungwa wa dhambi!”

24. Simoni akajibu, “Tafadhali, niombeeni kwa Bwana lisije likanipata lolote kati ya hayo mliyosema.”

25. Baada ya Petro na Yohane kutoa ushuhuda wao na kuutangaza ujumbe wa Bwana, walirudi Yerusalemu. Walipokuwa wanarudi walihubiri Habari Njema katika vijiji vingi vya Samaria.

26. Malaika wa Bwana alimwambia Filipo, “Jitayarishe uende kusini kupitia njia inayotoka Yerusalemu kwenda Gaza.” (Njia hiyo hupita jangwani).

Kusoma sura kamili Matendo 8