Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 8:30-40 Biblia Habari Njema (BHN)

30. Filipo akakimbilia karibu na gari, akamsikia huyo mtu akisoma katika kitabu cha nabii Isaya. Hapo Filipo akamwuliza, “Je, unaelewa hayo unayosoma?”

31. Huyo mtu akamjibu, “Ninawezaje kuelewa bila mtu kuniongoza?” Hapo akamwalika Filipo apande juu, aketi pamoja naye.

32. Basi, sehemu ya Maandiko Matakatifu aliyokuwa anasoma ilikuwa hii:“Alikuwa kama kondoo anayepelekwa kuchinjwa;kimya kama vile mwanakondoo anapokatwa manyoya,yeye hakutoa sauti hata kidogo.

33. Alifedheheshwa na kunyimwa haki.Hakuna atakayeweza kuongea juu ya kizazi chake,kwa maana maisha yake yameondolewa duniani.”

34. Huyo Mwethiopia akamwambia Filipo, “Niambie, huyu nabii anasema juu ya nini? Anasema mambo haya juu yake yeye mwenyewe au juu ya mtu mwingine?”

35. Basi, Filipo akianzia na sehemu hiyo ya Maandiko Matakatifu, akamweleza Habari Njema juu ya Yesu.

36. Walipokuwa bado wanaendelea na safari, walifika mahali penye maji, na huyo ofisa akasema, “Mahali hapa pana maji; je, kuna chochote cha kunizuia nisibatizwe?” [

37. Filipo akasema, “Kama unaamini kwa moyo wako wote unaweza kubatizwa.” Naye akajibu, “Naam, ninaamini kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu.”]

38. Basi, huyo ofisa akaamuru lile gari lisimame; na wote wawili, Filipo na huyo towashi wakashuka majini, naye Filipo akambatiza.

39. Walipotoka majini Roho wa Bwana akamfanya Filipo atoweke. Na huyo towashi hakumwona tena; lakini akaendelea na safari yake mwenye furaha.

40. Filipo akajikuta yuko Azoto, akapita katika miji yote akihubiri Injili mpaka alipofika Kaisarea.

Kusoma sura kamili Matendo 8