Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 7:39-54 Biblia Habari Njema (BHN)

39. “Lakini yeye ndiye babu zetu waliyekataa kumsikiliza; walimsukuma kando, wakatamani kurudi Misri.

40. Walimwambia Aroni: ‘Tutengenezee miungu itakayotuongoza njiani, maana hatujui yaliyompata huyo Mose aliyetuongoza kutoka Misri!’

41. Hapo ndipo walipojitengenezea sanamu ya ndama, wakaitambikia na kukifanyia sherehe kitu ambacho ni kazi ya mikono yao wenyewe.

42. Lakini Mungu aliondoka kati yao, akawaacha waabudu nyota za anga, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha manabii:‘Enyi watu wa Israeli!Si mimi mliyenitolea tambiko na sadakakwa miaka arubaini kule jangwani!

43. Nyinyi mlikibeba kibanda cha mungu Moloki,na sanamu ya nyota ya mungu wenu Refani.Sanamu mlizozifanya ndizo mlizoabudu.Kwa sababu hiyo nitawapeleka mateka mbali kupita Babuloni!’

44. Kule jangwani babu zetu walikuwa na lile hema la maamuzi. Lilitengenezwa kama Mungu alivyomwambia Mose alifanye; nakala kamili ya kile alichooneshwa.

45. Kisha babu zetu walilipokezana wao kwa wao mpaka wakati wa Yoshua, walipoinyakua ile nchi kutoka kwa mataifa ambayo Mungu aliyafukuza mbele yao. Hapo lilikaa mpaka nyakati za Daudi.

46. Daudi alipata upendeleo kwa Mungu, akamwomba Mungu ruhusa ya kumjengea makao yeye aliye Mungu wa Yakobo.

47. Lakini Solomoni ndiye aliyemjengea Mungu nyumba.

48. “Hata hivyo, Mungu Mkuu haishi katika nyumba zilizojengwa na binadamu; kama nabii asemavyo:

49. ‘Bwana asema:Mbingu ni kiti changu cha enzina dunia ni kiti changu cha kuwekea miguu.

50. Ni nyumba ya namna gani basi mnayoweza kunijengea,na ni mahali gani nitakapopumzika?Vitu hivi vyote ni mimi nimevifanya, au sivyo?’

51. “Enyi wakaidi wakuu! Mioyo na masikio yenu ni kama ya watu wa mataifa. Nyinyi ni kama babu zenu. Siku zote mnampinga Roho Mtakatifu.

52. Je, yuko nabii yeyote ambaye babu zenu hawakumtesa? Waliwaua hao Mungu aliowatuma watangaze kuja kwake yule Mwenye Haki. Na sasa, nyinyi mmemsaliti, mkamuua.

53. Nyinyi mliipokea ile sheria iliyoletwa kwenu na Malaika, lakini hamkuitii.”

54. Wale wazee wa Baraza waliposikia hayo, walighadhibika sana, wakamsagia meno kwa hasira.

Kusoma sura kamili Matendo 7