Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 7:24-38 Biblia Habari Njema (BHN)

24. Huko alimwona mmoja wao akitendewa vibaya, akaenda kumwokoa, na kwa kulipiza kisasi, akamuua yule Mmisri. (

25. Alidhani kwamba Waisraeli wenzake wangeelewa kwamba Mungu angemtumia yeye kuwakomboa, lakini hawakuelewa hivyo).

26. Kesho yake, aliwaona Waisraeli wawili wakipigana, akajaribu kuwapatanisha akisema: ‘Nyinyi ni ndugu; kwa nini basi, kutendeana vibaya nyinyi kwa nyinyi?’

27. Yule aliyekuwa anampiga mwenzake alimsukuma Mose kando akisema: ‘Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wetu?

28. Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?’

29. Baada ya kusikia hayo, Mose alikimbia, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani na huko akapata watoto wawili.

30. “Miaka arubaini ilipotimia, malaika wa Bwana alimtokea Mose katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto kule jangwani karibu na mlima Sinai.

31. Mose alistaajabu sana kuona tukio hilo hata akasogea karibu ili achungulie; lakini alisikia sauti ya Bwana:

32. ‘Mimi ni Mungu wa babu zako, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo!’ Mose akatetemeka kwa hofu na wala hakuthubutu kutazama zaidi.

33. Bwana akamwambia: ‘Vua viatu vyako maana hapa unaposimama ni mahali patakatifu.

34. Nimeyaona mabaya wanayotendewa watu wangu kule Misri. Nimesikia kilio chao, nami nimekuja kuwaokoa. Basi sasa, nitakutuma Misri.’

35. “Huyu Mose ndiye yule watu wa Israeli waliyemkataa waliposema: ‘Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wetu?’ Kwa njia ya yule malaika aliyemtokea katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto, Mungu alimtuma Mose huyo awe kiongozi na mkombozi.

36. Ndiye aliyewaongoza wale watu watoke Misri kwa kufanya miujiza na maajabu katika nchi ya Misri, katika bahari ya Shamu na jangwani, kwa muda wa miaka arubaini.

37. Mose ndiye aliyewaambia watu wa Israeli: ‘Mungu atawateulieni nabii kama mimi miongoni mwa ndugu zenu nyinyi wenyewe.’

38. Waisraeli walipokusanyika kule jangwani, Mose ndiye aliyekuwako huko kama mjumbe kati ya hao wazee wetu na yule malaika aliyeongea naye mlimani Sinai. Ndiye aliyekabidhiwa yale maneno ya uhai atupe sisi.

Kusoma sura kamili Matendo 7