Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 6:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Baadaye, idadi ya wanafunzi ilipokuwa inazidi kuongezeka, kulitokea manunguniko kati ya waumini walioongea Kigiriki na wale walioongea Kiebrania. Wale walioongea Kigiriki walinungunika kwamba wajane wao walikuwa wanasahauliwa katika ugawaji wa mahitaji ya kila siku.

2. Kwa hiyo, mitume kumi na wawili waliita jumuiya yote ya wanafunzi, wakasema, “Si vizuri sisi tuache kulihubiri neno la Mungu ili tushughulikie ugawaji wa mahitaji.

3. Hivyo, ndugu zetu, chagueni miongoni mwenu watu saba wenye sifa njema, waliojawa na Roho na wenye hekima; nasi tutawakabidhi jukumu hilo.

4. Sisi, lakini, tutashughulika na sala na kazi ya kuhubiri neno la Mungu.”

5. Jambo hilo likaipendeza jumuiya yote ya waumini. Wakawachagua Stefano, mtu mwenye imani kubwa na mwenye kujaa Roho Mtakatifu, Filipo, Prokoro, Nikanori, Timona, Parmena na Nikolao wa Antiokia ambaye wakati mmoja alikuwa ameongokea dini ya Kiyahudi.

6. Wakawaweka mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono.

7. Neno la Mungu likazidi kuenea na idadi ya waumini huko Yerusalemu ikaongezeka zaidi, na kundi kubwa la makuhani wakaipokea imani.

Kusoma sura kamili Matendo 6