Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 3:7-22 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Halafu, akamshika mkono wa kulia, akamwinua. Papo hapo miguu na magoti yake yakapata nguvu.

8. Akaruka, akasimama na kuanza kutembea. Halafu akaingia pamoja nao hekaluni, akitembea na kurukaruka huku akimtukuza Mungu.

9. Watu wote waliokuwa hapo walimwona akitembea na kumsifu Mungu.

10. Walipomtambua kuwa ndiye yule aliyekuwa anaombaomba karibu na ule “Mlango Mzuri” wa hekalu, wakashangaa mno hata wasiweze kuelewa yaliyompata.

11. Watu wote, wakiwa na mshangao mkubwa, wakaanza kukimbilia mahali palipoitwa “Ukumbi wa Solomoni,” ambapo yule mtu alikuwa bado anaandamana na Petro na Yohane.

12. Basi, Petro alipowaona watu hao akawaambia, “Wananchi wa Israeli, kwa nini mnashangazwa na jambo hili? Mbona mnatukodolea macho kana kwamba ni kwa nguvu zetu au utakatifu wetu sisi wenyewe tumemfanya mtu huyu aweze kutembea?

13. Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, Mungu wa babu zetu amemtukuza mtumishi wake Yesu. Yeye ndiye yuleyule mliyemtia mikononi mwa wakuu na kumkataa mbele ya Pilato hata baada ya Pilato kuamua kumwacha huru.

14. Alikuwa mtakatifu na mwema; lakini nyinyi mlimkataa, mkataka mtu mwingine aliyekuwa muuaji afunguliwe.

15. Basi, mlimuua yule ambaye ni chanzo cha uhai. Lakini Mungu alimfufua, na sisi ni mashahidi wa tukio hilo.

16. Jina la Yesu na imani katika jina hilo ndivyo vilivyompa nguvu mtu huyu mnayemwona na kumfahamu. Imani kwa Yesu ndiyo iliyomponya kabisa mtu huyu kama mnavyoona nyote.

17. “Sasa ndugu zangu, mnafahamu kwamba nyinyi na wakuu wenu mlitenda hayo kwa sababu ya kutokujua kwenu.

18. Lakini ndivyo Mungu alivyotimiza yale aliyotangaza zamani kwa njia ya manabii wote, kwamba ilikuwa lazima Kristo wake ateseke.

19. Basi, tubuni, mkamrudie Mungu ili yeye afute dhambi zenu.

20. Fanyeni hivyo ili Bwana awape nyakati za kuburudika rohoni na kuwaletea yule Kristo aliyemteua ambaye ndiye Yesu.

21. Ni lazima yeye abaki huko mbinguni mpaka utakapofika wakati wa kurekebishwa vitu vyote, kama Mungu alivyosema kwa njia ya manabii wake watakatifu wa tangu zamani.

22. Kwa maana Mose alisema, ‘Bwana Mungu wenu atawapelekeeni nabii kama mimi kutoka kati yenu nyinyi wenyewe.

Kusoma sura kamili Matendo 3