Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 28:17-23 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Baada ya siku tatu, Paulo aliwaita pamoja viongozi wa Kiyahudi wa mahali hapo. Walipokusanyika, Paulo aliwaambia, “Wananchi wenzangu, mimi, ingawa sikufanya chochote kibaya wala kupinga desturi za wazee wetu, nilitiwa nguvuni kule Yerusalemu na kutiwa mikononi mwa Waroma.

18. Waliponihoji na kuona kwamba sikuwa na hatia yoyote, walitaka kuniachia.

19. Lakini Wayahudi wengine walipinga jambo hilo, nami nikalazimika kukata rufani kwa Kaisari, ingawa sikuwa na chochote cha kuwashtaki wananchi wenzangu.

20. Ni kwa sababu hiyo nimeomba kuonana na kuongea nanyi, maana nimefungwa minyororo hii kwa sababu ya tumaini lile la Israeli.”

21. Wao wakamwambia, “Sisi hatujapokea barua yoyote kutoka Yudea, wala hakuna ndugu yeyote aliyefika hapa na kutoa habari rasmi au kusema chochote kibaya juu yako.

22. Lakini tunafikiri inafaa tusikie kutoka kwako mwenyewe mambo yaliyo kichwani mwako. Kwa maana tujualo sisi kuhusu hicho kikundi ni kwamba kinapingwa kila mahali.”

23. Basi, walipanga naye siku kamili ya kukutana, na wengi wakafika huko alikokuwa anakaa. Tangu asubuhi mpaka jioni Paulo aliwaeleza na kuwafafanulia juu ya ufalme wa Mungu, akijaribu kuwafanya wakubali habari juu ya Yesu kwa kutumia sheria na maandiko ya manabii.

Kusoma sura kamili Matendo 28