Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 24:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Baada ya siku tano, kuhani mkuu Anania aliwasili Kaisarea pamoja na wazee kadhaa na wakili mmoja wa sheria aitwaye Tertulo. Walimwendea yule mkuu wa mkoa wakamweleza mashtaka yao juu ya Paulo.

2. Paulo aliitwa, na Tertulo akafungua mashtaka hivi:“Mheshimiwa Felisi, uongozi wako bora umeleta amani kubwa na marekebisho ya lazima yanafanywa kwa manufaa ya taifa letu.

3. Tunalipokea jambo hili kwa furaha daima na kutoa shukrani nyingi kwako kila mahali.

4. Lakini, bila kupoteza wakati wako zaidi, tunakusihi kwa wema wako, usikilize taarifa yetu fupi.

5. Tumegundua kwamba mtu huyu ni wa hatari mno. Yeye huanzisha ghasia kati ya Wayahudi kila mahali duniani na pia ni kiongozi wa kile chama cha Wanazareti.

6. Tena alijaribu kulikufuru hekalu, nasi tukamtia nguvuni. [Tulitaka kumhukumu kufuatana na sheria yetu.

7. Lakini Lusia, mkuu wa jeshi, aliingilia kati, akamchukua kwa nguvu kutoka mikononi mwetu.

8. Kisha akaamuru washtaki wake waje mbele yako.] Kama ukimhoji wewe mwenyewe, utaweza kubainisha mambo haya yote tunayomshtaki kwayo.”

9. Nao Wayahudi waliunga mkono mashtaka hayo wakisema kwamba hayo yote yalikuwa kweli.

10. Basi, mkuu wa mkoa alimwashiria Paulo aseme. Naye Paulo akasema, “Nafurahi kujitetea mbele yako nikijua kwamba umekuwa hakimu wa taifa hili kwa miaka mingi.

11. Unaweza kujihakikishia kwamba si zaidi ya siku kumi na mbili tu zimepita tangu nilipokwenda kuabudu Yerusalemu.

12. Wayahudi hawakunikuta nikijadiliana na mtu yeyote. Hawakunikuta nikichochea watu hekaluni, wala katika masunagogi yao, wala mahali pengine popote katika mji huo.

13. Wala hawawezi kuthibitisha mashtaka waliyotoa juu yangu.

Kusoma sura kamili Matendo 24