Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 23:4-13 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Watu waliokuwa wamesimama pale wakamwambia Paulo, “Unamtukana kuhani mkuu wa Mungu!”

5. Paulo akajibu, “Ndugu zangu, sikujua kama yeye ni kuhani mkuu. Maana Maandiko yasema hivi: ‘Usiseme vibaya juu ya mtawala wa watu wako.’”

6. Wakati huo Paulo alikwisha tambua kwamba sehemu moja ya wanabaraza wale ilikuwa ni Masadukayo na nyingine Mafarisayo. Basi, alipaza sauti yake mbele ya Baraza, “Ndugu zangu, mimi ni Mfarisayo, mwana wa Mfarisayo. Mimi nimeletwa mahakamani kwa kuwa ninatumaini kwamba wafu watafufuka.”

7. Baada ya kusema hivyo, mzozo mkali ulitokea kati ya Mafarisayo na Masadukayo na mkutano ukagawanyika sehemu mbili.

8. Kisa chenyewe kilikuwa hiki, Masadukayo hushikilia kwamba wafu hawafufuki, hakuna malaika, na roho nazo hazipo. Lakini Mafarisayo husadiki hayo yote matatu.

9. Kelele ziliongezeka na baadhi ya waalimu wa sheria wa kikundi cha Mafarisayo walisimama na kutoa malalamiko yao kwa nguvu: “Hatuoni chochote kilicho kiovu katika mtu huyu; huenda ikawa kwamba roho au malaika ameongea naye.”

10. Mzozo ulizidi kuwa mwingi hata mkuu wa jeshi akaogopa kwamba Paulo angeraruliwa vipandevipande. Kwa hiyo, aliwaamuru askari wake kuingia kati ya lile kundi, wamtoe Paulo na kumrudisha ndani ya ngome.

11. Usiku uliofuata, Bwana alisimama karibu na Paulo, akamwambia, “Jipe moyo! Umenishuhudia hapa Yerusalemu, utafanya vivyo hivyo mjini Roma.”

12. Kulipokucha, Wayahudi walifanya kikao cha faragha. Wakala kiapo: “Hatutakula wala kunywa mpaka tutakapokuwa tumekwisha muua Paulo.”

13. Watu zaidi ya arubaini ndio waliokula njama kufanya hivyo.

Kusoma sura kamili Matendo 23