Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 22:22-30 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Mpaka hapa, wale watu walikuwa wanamsikiliza, lakini aliposema maneno haya, walianza kusema kwa sauti kubwa, “Mwondoe duniani! Mtu wa namna hiyo hastahili kuishi.”

23. Waliendelea kupayukapayuka huku wakitikisa makoti yao na kurusha vumbi angani.

24. Mkuu wa jeshi aliwaamuru watu wake wampeleke Paulo ndani ya ngome, akawaambia wamchape viboko ili wapate kujua kisa cha Wayahudi kumpigia kelele.

25. Lakini walipokwisha mfunga ili wamchape viboko, Paulo alimwuliza jemadari mmoja aliyesimama hapo, “Je, ni halali kwenu kumpiga viboko raia wa Roma kabla hajahukumiwa?”

26. Yule jemadari aliposikia hayo, alimpasha habari mkuu wa jeshi akisema, “Unataka kufanya nini? Mtu huyu ni raia wa Roma!”

27. Basi, mkuu wa jeshi alimwendea Paulo, akamwambia, “Niambie; je, wewe ni raia wa Roma?” Paulo akamjibu, “Naam.”

28. Mkuu wa jeshi akasema, “Mimi nami nimekuwa raia wa Roma kwa kulipa gharama kubwa.” Paulo akasema, “Lakini mimi ni raia wa Roma kwa kuzaliwa.”

29. Wale watu ambao walikuwa tayari kumchunguza Paulo walitoweka mara. Hata yule mkuu wa jeshi aliogopa alipojua kwamba Paulo ni raia wa Roma na kwamba alikuwa amekwisha mfunga minyororo.

30. Kesho yake, mkuu wa jeshi alitaka kujua mashtaka kamili ambayo Wayahudi walikuwa wamemwekea Paulo. Hivyo, alimfungua Paulo minyororo, akaamuru makuhani wakuu na Baraza lote wafanye kikao. Kisha alimleta Paulo, akamsimamisha mbele ya Baraza.

Kusoma sura kamili Matendo 22