Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 21:4-21 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Tulikuta waumini huko, tukakaa pamoja nao kwa muda wa juma moja. Waumini hao wakawa wanaongea kwa nguvu ya Roho, wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu.

5. Lakini muda wetu ulipokwisha tuliondoka. Wote pamoja na wanawake na watoto wao walitusindikiza mpaka nje ya mji. Tulipofika pwani, sote tulipiga magoti tukasali.

6. Kisha tuliagana; sisi tukapanda meli, nao wakarudi makwao.

7. Sisi tuliendelea na safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai ambapo tuliwasalimu ndugu zetu, tukakaa nao siku moja.

8. Kesho yake tuliondoka tukaenda Kaisarea. Huko tulikwenda nyumbani kwa mhubiri Filipo. Yeye alikuwa mmoja wa wale saba waliochaguliwa kule Yerusalemu.

9. Alikuwa na binti wanne ambao walikuwa na kipaji cha unabii.

10. Baada ya kukaa huko siku kadhaa, nabii mmoja aitwaye Agabo alifika kutoka Yudea.

11. Alitujia, akachukua mkanda wa Paulo, akajifunga mikono na miguu, akasema, “Roho Mtakatifu asema hivi: ‘Wayahudi kule Yerusalemu watamfunga namna hii mtu mwenye mkanda huu na kumtia mikononi mwa watu wa mataifa.’”

12. Tuliposikia hayo, sisi na wale watu wengine waliokuwa hapo tulimsihi Paulo asiende Yerusalemu.

13. Lakini yeye alijibu, “Mnataka kufanya nini? Mnataka kuvunja moyo wangu kwa machozi? Niko tayari siyo tu kutiwa ndani kule Yerusalemu, ila hata kufa kwa ajili ya Bwana Yesu.”

14. Tuliposhindwa kumshawishi tulinyamaza, tukasema tu: “Atakalo Bwana lifanyike!”

15. Baada ya kukaa pale kwa muda, tulifunga mizigo yetu, tukaendelea na safari kwenda Yerusalemu.

16. Baadhi ya wale wafuasi wa Kaisarea walikwenda pamoja nasi, wakatupeleka nyumbani kwa Mnasoni ambaye tulikuwa tunakwenda kukaa naye kwa muda. Mnasoni alikuwa mwenyeji wa Kupro na alikuwa amekuwa mwaamini kwa siku nyingi.

17. Tulipofika Yerusalemu, ndugu waumini walitupokea vizuri sana.

18. Kesho yake Paulo alikwenda pamoja nasi kumwamkia Yakobo, na wazee wote wa kanisa walikuwapo pia.

19. Baada ya kuwasalimu, Paulo aliwapa taarifa kamili kuhusu yote Mungu aliyokuwa ametenda kati ya watu wa mataifa kwa njia ya utumishi wake.

20. Waliposikia hayo, walimtukuza Mungu. Kisha wakamwambia Paulo, “Ndugu, unaweza kuona kwamba kuna maelfu ya Wayahudi ambao sasa wamekuwa waumini na wote hao wanazingatia sheria.

21. Wamepata habari zako kwamba umekuwa ukiwafundisha Wayahudi wanaoishi miongoni mwa watu wa mataifa mengine kuwa wasiijali sheria, wasiwatahiri watoto wao na kwamba wasizifuate mila za Wayahudi.

Kusoma sura kamili Matendo 21