Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 20:4-16 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Sopatro, mwana wa Pirho, kutoka Berea, aliandamana naye; pia Aristarko na Sekundo kutoka Thesalonike, Gayo kutoka Derbe, Timotheo, Tukiko na Trofimo wa mkoa wa Asia.

5. Hao walitutangulia na kutungojea kule Troa.

6. Sisi, baada ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, tulipanda meli kutoka Filipi na baada ya siku tatu tukawafikia kule Troa. Huko tulikaa kwa muda wa juma moja.

7. Jumamosi jioni tulikutana ili kumega mkate. Kwa vile Paulo alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliwahutubia watu na kuendelea kuongea nao hadi usiku wa manane.

8. Katika chumba tulimokuwa, ghorofani, kulikuwa na taa nyingi zinawaka.

9. Kijana mmoja aitwaye Eutuko alikuwa ameketi dirishani wakati Paulo alipokuwa anaendelea kuhutubu. Eutuko alianza kusinzia kidogokidogo na hatimaye usingizi ukambana, akaanguka chini kutoka ghorofa ya tatu. Wakamwokota amekwisha kufa.

10. Lakini Paulo alishuka chini, akainama, akamkumbatia na kusema, “Msiwe na wasiwasi maana kuna uhai bado ndani yake.”

11. Kisha akapanda tena ghorofani, akamega mkate, akala. Aliendelea kuhubiri kwa muda mrefu hadi alfajiri, halafu akaondoka.

12. Wale watu walimchukua yule kijana hadi nyumbani akiwa mzima kabisa, wakapata kitulizo kikubwa.

13. Sisi tulipanda meli tukatangulia kwenda Aso ambako tungemchukua Paulo. Ndivyo alivyopanga; maana alitaka kufika huko kwa kupitia nchi kavu.

14. Basi, alitukuta kule Aso, tukampandisha melini, tukaenda Mitulene.

15. Kutoka huko tulisafiri tukafika Kio kesho yake. Siku ya pili, tulitia nanga Samo na kesho yake tukafika Mileto.

16. Paulo alikuwa amekusudia kuendelea na safari kwa meli bila kupitia Efeso ili asikawie zaidi huko Asia. Alikuwa na haraka ya kufika Yerusalemu kwa sikukuu ya Pentekoste kama ingewezekana.

Kusoma sura kamili Matendo 20