Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 2:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Siku ya Pentekoste ilipofika, waumini wote walikuwa wamekusanyika mahali pamoja.

2. Ghafla, sauti ikasikika kutoka angani; sauti iliyokuwa kama ya upepo mkali, ikaijaza ile nyumba yote walimokuwa wamekaa.

3. Kisha, vikatokea vitu vilivyoonekana kama ndimi za moto, vikagawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao.

4. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha mbalimbali kadiri Roho alivyowawezesha.

5. Na huko Yerusalemu walikuwako Wayahudi, watu wamchao Mungu, waliotoka katika kila nchi duniani.

6. Waliposikia sauti hiyo, kundi kubwa la watu lilikusanyika. Wote walishtuka sana kwani kila mmoja wao aliwasikia hao waumini wakisema kwa lugha yake mwenyewe.

7. Walistaajabu na kushangaa wakisema, “Je, hawa wote tunaowasikia wakisema hivi, si wenyeji wa Galilaya?

8. Imekuwaje, basi, kwamba kila mmoja wetu anawasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe?

9. Baadhi yetu ni Waparthi, Wamedi na Waelamu; wengine ni wenyeji wa Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na Asia,

10. Frugia na Pamfulia, Misri na sehemu za Libia karibu na Kurene; wengine wetu ni wageni kutoka Roma,

11. Wayahudi na watu walioongokea dini ya Kiyahudi; wengine wametoka Krete na Arabia. Sisi sote tunasikia wakisema kwa lugha zetu wenyewe mambo makuu ya Mungu.”

12. Wote walishangaa na kufadhaika huku wakiulizana, “Hii ina maana gani?”

13. Lakini wengine wakawadhihaki wakisema, “Watu hawa wamelewa divai mpya!”

14. Lakini Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja akaanza kuwahutubia watu kwa sauti kubwa: “Ndugu Wayahudi nanyi nyote mnaokaa hapa Yerusalemu, sikilizeni kwa makini maneno yangu.

15. Watu hawa hawakulewa kama mnavyodhani; mbona ni saa tatu tu asubuhi?

Kusoma sura kamili Matendo 2