Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 13:43-52 Biblia Habari Njema (BHN)

43. Mkutano huo ulipomalizika, Wayahudi wengi na watu wa mataifa mengine waliokuwa wameongokea dini ya Kiyahudi waliwafuata Paulo na Barnaba. Hao mitume waliongea nao, wakawatia moyo waendelee kuishi wakitegemea neema ya Mungu.

44. Siku ya Sabato iliyofuata, karibu kila mtu katika ule mji alikuja kusikiliza neno la Bwana.

45. Lakini Wayahudi walipoliona hilo kundi la watu walijaa wivu, wakapinga alichokuwa anasema Paulo na kumtukana.

46. Hata hivyo, Paulo na Barnaba waliongea kwa uhodari zaidi, wakasema, “Ilikuwa ni lazima neno la Mungu liwafikieni nyinyi kwanza; lakini kwa kuwa mmelikataa na kujiona hamstahili uhai wa milele, basi, tunawaacheni na kuwaendea watu wa mataifa mengine.

47. Maana Bwana alituagiza hivi:‘Nimekuweka wewe uwe mwanga kwa watu wa mataifa,ili uwaletee watu wokovu pote ulimwenguni.’”

48. Watu wa mataifa mengine waliposikia jambo hilo walifurahi, wakausifu ujumbe wa Mungu; na wale waliokuwa wamechaguliwa kupata uhai wa milele, wakawa waumini.

49. Neno la Bwana likaenea kila mahali katika sehemu ile.

50. Lakini Wayahudi waliwachochea wanawake wa tabaka ya juu wa mataifa mengine ambao walikuwa wacha Mungu, na wanaume maarufu wa mji huo. Wakaanza kuwatesa Paulo na Barnaba, wakawafukuza kutoka katika eneo lao.

51. Basi, mitume wakayakunguta mavumbi yaliyokuwa katika miguu yao kama onyo, kisha wakaenda Ikonio.

52. Lakini hao wafuasi walikuwa wamejaa furaha na Roho Mtakatifu.

Kusoma sura kamili Matendo 13