Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 13:29-46 Biblia Habari Njema (BHN)

29. Na baada ya kutekeleza yote yaliyokuwa yameandikwa kumhusu yeye, walimshusha kutoka msalabani, wakamweka kaburini.

30. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu.

31. Naye, kwa siku nyingi, aliwatokea wale waliofuatana naye kutoka Galilaya mpaka Yerusalemu. Hao ndio walio sasa mashahidi wake kwa watu wa Israeli.

32. Nasi tumekuja hapa kuwaleteeni Habari Njema: Jambo lile Mungu alilowaahidia babu zetu,

33. amelitimiza sasa kwa ajili yetu sisi wajukuu wao kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu. Kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili:‘Wewe ni Mwanangu,mimi leo nimekuwa baba yako.’

34. Na juu ya kumfufua kutoka kwa wafu, asipate tena kurudi huko na kuoza, Mungu alisema hivi:‘Nitakupa baraka takatifu na za kweli nilizomwahidia Daudi.’

35. Naam, na katika sehemu nyingine za Zaburi asema:‘Hutamwacha Mtakatifu wako aoze.’

36. Sasa, Daudi mwenyewe alitimiza matakwa ya Mungu wakati wake; kisha akafa na kuzikwa karibu na wazee wake, na mwili wake ukaoza.

37. Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka wafu hakupata kuoza.

38. Kwa hiyo, jueni, ndugu zangu, kwamba kwa njia ya mtu huyu ujumbe kuhusu kusamehewa dhambi unahubiriwa kwenu;

39. na ya kwamba kila mmoja anayemwamini Yesu anasamehewa dhambi zote, jambo ambalo halingewezekana kwa njia ya sheria.

40. Jihadharini basi, msije mkapatwa na yale yaliyosemwa na manabii:

41. ‘Sikilizeni enyi wenye madharau,shangaeni mpotee!Kwa maana kitu ninachofanya sasa, nyakati zenu,ni kitu ambacho hamtakiamini hata kama mtu akiwaelezeni.’”

42. Paulo na Barnaba walipokuwa wanatoka katika lile sunagogi, wale watu waliwaalika waje tena siku ya Sabato iliyofuata, waongee zaidi juu ya mambo hayo.

43. Mkutano huo ulipomalizika, Wayahudi wengi na watu wa mataifa mengine waliokuwa wameongokea dini ya Kiyahudi waliwafuata Paulo na Barnaba. Hao mitume waliongea nao, wakawatia moyo waendelee kuishi wakitegemea neema ya Mungu.

44. Siku ya Sabato iliyofuata, karibu kila mtu katika ule mji alikuja kusikiliza neno la Bwana.

45. Lakini Wayahudi walipoliona hilo kundi la watu walijaa wivu, wakapinga alichokuwa anasema Paulo na kumtukana.

46. Hata hivyo, Paulo na Barnaba waliongea kwa uhodari zaidi, wakasema, “Ilikuwa ni lazima neno la Mungu liwafikieni nyinyi kwanza; lakini kwa kuwa mmelikataa na kujiona hamstahili uhai wa milele, basi, tunawaacheni na kuwaendea watu wa mataifa mengine.

Kusoma sura kamili Matendo 13