Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 10:12-22 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Ndani ya shuka hiyo kulikuwa na kila aina ya wanyama: Wanyama wenye miguu minne, wanyama watambaao na ndege wa angani.

13. Akasikia sauti ikimwambia: “Petro, amka uchinje, ule!”

14. Petro akajibu, “La, Bwana; mimi sijaonja kamwe chochote ambacho ni najisi au kichafu.”

15. Ile sauti ikasikika tena ikimwambia: “Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa!”

16. Jambo hili lilifanyika mara tatu, kisha ile shuka ikarudishwa juu mbinguni.

17. Petro alipokuwa bado anashangaa juu ya maana ya hayo maono aliyokuwa ameyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, baada ya kuigundua nyumba ya Simoni, walifika mlangoni,

18. wakaita kwa sauti: “Je, kuna mgeni humu aitwaye Simoni Petro?”

19. Petro alikuwa bado anajaribu kuelewa yale maono, na hapo Roho akamwambia, “Sikiliza! Kuna watu watatu hapa, wanakutafuta.

20. Shuka upesi na wala usisite kwenda pamoja nao kwa maana ni mimi niliyewatuma.”

21. Basi, Petro akateremka chini, akawaambia hao watu, “Mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja?”

22. Wao wakamjibu, “Jemadari Kornelio ambaye ni mtu mwema, mcha Mungu na mwenye kuheshimika mbele ya Wayahudi wote, ametutuma. Aliambiwa na malaika mtakatifu akualike nyumbani kwake ili asikilize chochote ulicho nacho cha kusema.”

Kusoma sura kamili Matendo 10