Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 9:20-32 Biblia Habari Njema (BHN)

20. Wakampeleka. Mara tu huyo pepo alipomwona Yesu, alimtia mtoto kifafa, naye mtoto akaanguka chini, akagaagaa na kutoka povu kinywani. Yesu akamwuliza baba yake huyo mtoto,

21. “Amepatwa na mambo hayo tangu lini?” Naye akamjibu, “Tangu utoto wake.

22. Na mara nyingi pepo huyo amemwangusha motoni na majini, ili amwangamize kabisa. Basi, ikiwa waweza, utuhurumie na kutusaidia!”

23. Yesu akamwambia, “Ati ikiwa waweza! Mambo yote yanawezekana kwa mtu aliye na imani.”

24. Hapo, huyo baba akalia kwa sauti, “Naamini! Lakini imani yangu haitoshi, nisaidie.”

25. Yesu alipouona umati wa watu unaongezeka upesi mbele yake, alimkemea yule pepo mchafu “Pepo unayemfanya huyu mtoto kuwa bubu na kiziwi, nakuamuru, mtoke mtoto huyu wala usimwingie tena!”

26. Hapo huyo pepo alipaza sauti, akamwangusha huyo mtoto chini, kisha akamtoka. Mtoto alionekana kama maiti, hata wengine walisema, “Amekufa!”

27. Lakini Yesu akamshika mkono, akamwinua, naye akasimama.

28. Basi, Yesu alipoingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza kwa faragha, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?”

29. Naye akawaambia, “Pepo wa aina hii hawezi kutoka isipokuwa kwa sala.”

30. Yesu na wanafunzi wake waliondoka hapo, wakaendelea na safari kupitia wilaya ya Galilaya. Yesu hakupenda watu wajue alipokuwa,

31. kwa sababu alikuwa anawafundisha wanafunzi wake. Aliwaambia, “Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa watu ambao watamuua; lakini siku ya tatu baada ya kuuawa atafufuka.”

32. Wanafunzi hawakufahamu jambo hilo. Wakaogopa kumwuliza.

Kusoma sura kamili Marko 9