Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 8:25-36 Biblia Habari Njema (BHN)

25. Kisha Yesu akamwekea tena mikono machoni, naye akakaza macho, uwezo wake wa kuona ukamrudia, akaona kila kitu sawasawa.

26. Yesu akamwambia aende zake nyumbani na kumwamuru, “Usirudi kijijini!”

27. Kisha Yesu na wanafunzi wake walikwenda katika vijiji vya Kaisarea Filipi. Walipokuwa njiani, Yesu aliwauliza wanafunzi wake, “Watu wanasema mimi ni nani?”

28. Wakamjibu, “Wengine wanasema wewe ni Yohane Mbatizaji, wengine Elia na wengine mmojawapo wa manabii.”

29. Naye akawauliza, “Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?” Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Kristo.”

30. Kisha Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake.

31. Yesu alianza kuwafundisha wanafunzi wake kwamba ni lazima Mwana wa Mtu apatwe na mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na waalimu wa sheria. Kwamba atauawa, na baada ya siku tatu atafufuka.

32. Yesu aliwaambia jambo hilo waziwazi. Hapo, Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea.

33. Lakini Yesu akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro akisema, “Ondoka mbele yangu Shetani! Mawazo yako si ya kimungu ila ni ya kibinadamu.”

34. Kisha akauita umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Kama mtu yeyote anataka kuwa mfuasi wangu, lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.

35. Maana mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza, lakini mtu anayepoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema, atayaokoa.

36. Je, kuna faida gani mtu kuupata ulimwengu wote na kuyapoteza maisha yake?

Kusoma sura kamili Marko 8