Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 8:23-31 Biblia Habari Njema (BHN)

23. Yesu akamshika huyo kipofu mkono, akampeleka nje ya kijiji. Akamtemea mate machoni, akamwekea mikono, akamwuliza, “Je, unaweza kuona kitu?”

24. Huyo kipofu akatazama, akasema, “Ninawaona watu wanaoonekana kama miti inayotembea.”

25. Kisha Yesu akamwekea tena mikono machoni, naye akakaza macho, uwezo wake wa kuona ukamrudia, akaona kila kitu sawasawa.

26. Yesu akamwambia aende zake nyumbani na kumwamuru, “Usirudi kijijini!”

27. Kisha Yesu na wanafunzi wake walikwenda katika vijiji vya Kaisarea Filipi. Walipokuwa njiani, Yesu aliwauliza wanafunzi wake, “Watu wanasema mimi ni nani?”

28. Wakamjibu, “Wengine wanasema wewe ni Yohane Mbatizaji, wengine Elia na wengine mmojawapo wa manabii.”

29. Naye akawauliza, “Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?” Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Kristo.”

30. Kisha Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake.

31. Yesu alianza kuwafundisha wanafunzi wake kwamba ni lazima Mwana wa Mtu apatwe na mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na waalimu wa sheria. Kwamba atauawa, na baada ya siku tatu atafufuka.

Kusoma sura kamili Marko 8