Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 3:6-22 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Mara Mafarisayo wakatoka nje, wakafanya shauri pamoja na watu wa kikundi cha Herode jinsi ya kumwangamiza Yesu.

7. Yesu aliondoka hapo pamoja na wanafunzi wake, akaenda kando ya ziwa, na umati wa watu ukamfuata. Watu hao walikuwa wametoka Yerusalemu, Yudea,

8. Idumea, ngambo ya mto Yordani, Tiro na Sidoni. Watu hao wengi walimwendea Yesu kwa sababu ya kusikia mambo mengi aliyokuwa ameyatenda.

9. Yesu akawaambia wanafunzi wake wamtayarishie mashua moja, ili umati wa watu usije ukamsonga.

10. Alikuwa amewaponya watu wengi, na wagonjwa wote wakawa wanamsonga ili wapate kumgusa.

11. Na watu waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu walipomwona, walijitupa chini mbele yake na kupaza sauti, “Wewe ni Mwana wa Mungu!”

12. Lakini Yesu akawaamuru kwa ukali wasimjulishe kwa watu.

13. Yesu alipanda kilimani, akawaita wale aliowataka. Basi, wakamwendea,

14. naye akawateua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume, wakae naye, awatume kuhubiri

15. na wawe na uwezo wa kuwafukuza pepo.

16. Basi, hao kumi na wawili walioteuliwa ndio hawa: Simoni (ambaye Yesu alimpa jina, Petro),

17. Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo (Yesu aliwapa hawa ndugu wawili jina Boanerge, maana yake “Wanangurumo”),

18. Andrea na Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Thoma, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkanaani na

19. Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu.

20. Kisha Yesu alikwenda nyumbani. Umati wa watu ukakusanyika tena, hata Yesu na wafuasi wake wasiweze kupata nafasi ya kula chakula.

21. Basi, watu wa jamaa yake walipopata habari hiyo wakatoka kwenda kumchukua maana walikuwa wanasema kwamba ana wazimu.

22. Nao waalimu wa sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu, wakasema, “Ana Beelzebuli! Tena, anawafukuza pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo.”

Kusoma sura kamili Marko 3