Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 16:7-19 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Nendeni mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro ya kwamba anawatangulieni kule Galilaya. Huko mtamwona kama alivyowaambieni.”

8. Basi, wakatoka pale kaburini mbio, maana walitetemeka kwa hofu na kushangaa. Hawakumwambia mtu yeyote kitu, kwa sababu waliogopa mno.[

9. Yesu alipofufuka mapema Jumapili, alijionesha kwanza kwa Maria Magdalene, ambaye Yesu alikuwa amemtoa pepo wabaya saba.

10. Maria Magdalene akaenda, akawajulisha wale waliokuwa pamoja na Yesu, na wakati huo walikuwa wanaomboleza na kulia.

11. Lakini waliposikia ya kwamba Yesu yu hai na kwamba Maria Magdalene amemwona, hawakuamini.

12. Baadaye Yesu aliwatokea wanafunzi wawili akiwa na sura nyingine. Wanafunzi hao walikuwa wanakwenda shambani.

13. Nao pia wakaenda, wakawaambia wenzao. Hata hivyo hawakuamini.

14. Mwishowe Yesu aliwatokea wanafunzi kumi na mmoja walipokuwa pamoja mezani. Akawakemea sana kwa sababu ya kutoamini kwao na ukaidi wao, maana hawakuwaamini wale waliokuwa wamemwona baada ya kufufuka.

15. Basi, akawaambia, “Nendeni ulimwenguni kote mkahubiri Habari Njema kwa kila mtu.

16. Anayeamini na kubatizwa ataokolewa. Asiyeamini atahukumiwa.

17. Na ishara hizi zitaandamana na wale wanaoamini: Kwa jina langu watatoa pepo na watasema kwa lugha mpya.

18. Wakishika nyoka au wakinywa kitu chochote chenye sumu, hakitawadhuru. Watawawekea wagonjwa mikono, nao watapona.”

19. Basi, Bwana Yesu alipokwisha sema nao, akachukuliwa mbinguni, akaketi upande wa kulia wa Mungu.

Kusoma sura kamili Marko 16