Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 15:23-40 Biblia Habari Njema (BHN)

23. Wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini yeye alikataa kunywa.

24. Basi, wakamsulubisha, wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura waamue nani angepata nini.

25. Ilikuwa saa tatu asubuhi walipomsulubisha.

26. Na shtaka dhidi yake lilikuwa limeandikwa, “Mfalme wa Wayahudi.”

27. Pamoja naye waliwasulubisha wanyanganyi wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto. [

28. Hapo yakatimia Maandiko Matakatifu yanayosema, “Aliwekwa kundi moja na waovu.”]

29. Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana, wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Aha! Wewe mwenye kuvunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu!

30. Sasa, shuka msalabani ujiokoe mwenyewe!”

31. Nao makuhani wakuu pamoja na waalimu wa sheria walimdhihaki wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi!

32. Ati yeye ni Kristo, Mfalme wa Israeli! Basi, na ashuke kutoka msalabani ili tuone na kuamini.” Hata watu wale waliosulubiwa pamoja naye walimtukana.

33. Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa giza likaikumba nchi yote.

34. Saa tisa alasiri Yesu akalia kwa sauti kubwa, akasema, “Eloi, Eloi, lema sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

35. Baadhi ya watu waliosimama pale waliposikia hivyo, walisema, “Sikiliza! Anamwita Elia.”

36. Mtu mmoja akakimbia, akaichovya sifongo katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe akisema, “Hebu tuone kama Elia atakuja kumteremsha msalabani!”

37. Yesu akapaza sauti kubwa, akakata roho.

38. Basi, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu mpaka chini.

39. Jemadari mmoja aliyekuwa amesimama mbele yake alipoona kwamba Yesu alikata roho namna hiyo, akasema, “Kweli mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”

40. Walikuwako pia wanawake waliotazama kwa mbali, miongoni mwao akiwa Maria Magdalene, Salome, na Maria mama wa kina Yakobo mdogo na Yose.

Kusoma sura kamili Marko 15