Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 11:14-25 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Hapo akauambia mtini, “Tangu leo hata milele mtu yeyote asile matunda kwako.” Nao wanafunzi wake walisikia maneno hayo.

15. Basi, wakafika Yerusalemu. Yesu akaingia hekaluni akaanza kuwafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu humo. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilishana fedha, na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa.

16. Hakumruhusu mtu yeyote kupitia hekaluni akichukua kitu.

17. Kisha akawafundisha, “Imeandikwa: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa ajili ya mataifa yote!’ Lakini nyinyi mmeifanya kuwa pango la wanyanganyi!”

18. Makuhani wakuu na waalimu wa sheria waliposikia hayo, walianza kutafuta njia ya kumwangamiza. Lakini walimwogopa kwa sababu umati wa watu ulishangazwa na mafundisho yake.

19. Ilipokuwa jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka mjini.

20. Asubuhi na mapema, walipokuwa wanapita, waliuona ule mtini umenyauka wote, hata mizizi.

21. Petro aliukumbuka, akamwambia Yesu, “Mwalimu, tazama! Ule mtini ulioulaani, umenyauka!”

22. Yesu akawaambia, “Mwaminini Mungu.

23. Nawaambieni kweli, mtu akiuambia mlima huu: ‘Ngoka ukajitose baharini,’ bila kuona shaka moyoni mwake, ila akaamini kwamba mambo yote anayosema yanafanyika, atafanyiwa jambo hilo.

24. Kwa hiyo nawaambieni, mnaposali na kuomba kitu, aminini kwamba mmekipokea, nanyi mtapewa.

25. Mnaposimama kusali, msameheni kila mtu aliyewakosea chochote, ili Baba yenu aliye mbinguni awasamehe nyinyi makosa yenu.” [

Kusoma sura kamili Marko 11