Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 10:32-47 Biblia Habari Njema (BHN)

32. Basi, walikuwa njiani kwenda juu Yerusalemu, na Yesu alikuwa anawatangulia. Wanafunzi wake walijawa na hofu, na watu waliofuata waliogopa. Yesu akawachukua tena kando wale kumi na wawili, akaanza kuwaambia yale yatakayompata:

33. “Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na waalimu wa sheria, nao watamhukumu auawe na kumkabidhi kwa watu wa mataifa.

34. Nao watamdhihaki; watamtemea mate, watampiga mijeledi na kumuua. Lakini baada ya siku tatu atafufuka.”

35. Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu wakamwambia, “Mwalimu, tunataka utufanyie kitu tutakachokuomba.”

36. Yesu akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”

37. Wakamjibu, “Uturuhusu kuketi mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto katika utukufu wako.”

38. Yesu akawaambia, “Hamjui mnaomba nini! Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa, au kubatizwa kama nitakavyobatizwa?”

39. Wakamjibu, “Tunaweza.” Yesu akawaambia, “Kikombe nitakachokunywa mtakinywa kweli, na mtabatizwa kama nitakavyobatizwa.

40. Lakini ni nani atakayeketi kulia au kushoto kwangu si wajibu wangu kupanga bali nafasi hizo watapewa wale waliotayarishiwa.”

41. Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, walianza kuchukizwa na Yakobo na Yohane.

42. Hivyo, Yesu akawaita, akawaambia, “Mnajua kwamba wale wanaofikiriwa kuwa watawala wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, na wakuu hao huwamiliki watu wao.

43. Lakini kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkubwa kati yenu, sharti awe mtumishi wenu.

44. Anayetaka kuwa wa kwanza, sharti awe mtumishi wa wote.

45. Maana Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, ila kutumikia, na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi.”

46. Basi, wakafika Yeriko, naye Yesu alipokuwa anatoka katika mji huo akiwa na wanafunzi wake pamoja na umati mkubwa wa watu, kipofu, mwana wa Timayo aitwaye Bartimayo, alikuwa ameketi kando ya barabara, anaomba maskini.

47. Aliposikia kwamba ni Yesu wa Nazareti aliyekuwa anapita mahali hapo, alianza kupaza sauti, “Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!”

Kusoma sura kamili Marko 10