Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 9:11-27 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Lakini wale watu walipojua alikokwenda, walimfuata. Yesu akawakaribisha akawazungumzia juu ya ufalme wa Mungu, akawaponya wale waliohitaji kuponywa.

12. Jua lilipokuwa linaanza kutua, wale kumi na wawili walimwendea wakamwambia, “Waage watu waende kwenye vijiji na mashamba ya karibu, wakajipatie chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tulipo ni nyikani.”

13. Lakini Yesu akawaambia, “Wapeni nyinyi chakula.” Wakamjibu, “Hatuna chochote ila mikate mitano na samaki wawili. Labda twende wenyewe tukawanunulie chakula watu wote hawa!”

14. (Walikuwapo pale wanaume wapatao 5,000.) Basi, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Waambieni watu waketi katika makundi ya watu hamsinihamsini.”

15. Wanafunzi wakafanya walivyoambiwa, wakawaketisha wote.

16. Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akavibariki, akavimega, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu.

17. Watu wote wakala, wakashiba. Wakakusanya mabaki ya chakula, wakajaza vikapu kumi na viwili.

18. Siku moja, Yesu alikuwa anasali peke yake, na wanafunzi wake walikuwa karibu. Basi, akawauliza, “Watu wanasema mimi ni nani?”

19. Nao wakamjibu, “Wengine wanasema kuwa wewe ni Yohane Mbatizaji; wengine, Elia; wengine, mmojawapo wa manabii wa kale ambaye amefufuka.”

20. Hapo akawauliza, “Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?” Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo wa Mungu.”

21. Halafu Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari hiyo.

22. Akaendelea kusema kwamba ni lazima Mwana wa Mtu apate mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na waalimu wa sheria na kuuawa, lakini siku ya tatu atafufuliwa.

23. Kisha akawaambia watu wote, “Mtu yeyote akitaka kuwa mfuasi wangu, ni lazima ajikane nafsi yake, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate.

24. Maana, mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza; lakini anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayaokoa.

25. Je, kuna faida gani mtu kuupata utajiri wote wa dunia kwa kujipoteza au kujiangamiza yeye mwenyewe?

26. Mtu akinionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo wakati atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu.

27. Nawaambieni kweli, kuna wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona ufalme wa Mungu.”

Kusoma sura kamili Luka 9